Kutolewa hukumu ya kumtia nguvuni Trump; Azma ya Iran na Iraq kwa ajili ya kuadhibiwa wahusika wa mauaji ya makamanda wa muqawama

Sayyid Razi Imadi Faiq Zaidan, Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq ameeleza kuwa chombo cha mahakama cha nchi hiyo kimetoa hukumu ya kutiwa mbaroni Donald Trump rais wa zamani wa Marekani ambaye amekiri hadharani kutekeleza jinai hiyo ya mauaji dhidi ya makamanda wa ushindi.

Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na Abu Mahdi al Muhandes Naibu Mkuu wa Kikosi cha kujitoea cha wanamapambano wa Iraq cha al Hashdu Shaabi pamoja na wanajihadi wenzao kadhaa waliuliwa shahidi na Marekani alfajiri ya Januari 3 mwaka 2020 karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alitangaza hadharani kuwa yeye ndiye aliamuru kutekelezwa mauaji hayo ya kigaidi.

Ikiwa imepita miaka mitatu sasa tangu kujiri jinai hiyo ya Marekani, chombo cha mahakama cha Iraq kimetangaza kuwa tayari kimetoa hukumu ya kumtia nguvuni Donald Trump. Suala kwamba je serikali ya Iraq inao uwezo wa kutekeleza hukumu hiyo au la; au kwamba serikali ya Marekani itakubaliana na kwenda sambamba na Iraq kuhusiana na kadhia hii au la; ni jambo lililo na umuhimu mkubwa hivi sasa. Uamuzi huu tajwa aidha una umuhimu katika pande nyingine kadhaa.

Umuhimu wa kwanza ni huu kuwa, hukumu hii imethibitisha kuwa Donald Trump ni mtenda jinai na wakati huo huo suala hili limebainishwa na afisa wa ngazi ya juu zaidi wa chombo cha mahakama cha Iraq. Jaji Faiq Zaidan Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq amesema katika marasimu yaliyofanyika huko Baghdad ya kuwaenzi na kuadhimisha kutimia mwaka wa tatu tangu kuuliwa kigaidi Mashahidi Qassim Soleimani na Abu Mahdi al Muhandes kwamba janga la kuuliwa shahidi makamanda wa ushindi ilikuwa jinai ya kioga na isiyo na msingi wowote wa kisheria.

Umuhimu mwingine wa hukumu iliyotolewa ya kumtia nguvuni Trump ni huu kuwa hukumu hiyo inathibitisha kwamba Marekani, nchi inayodai eti kupambana na ugaidi yenyewe ni moja ya waungaji mkono wakuu wa ugaidi duniani. Hii ni kwa sababu, amri ya kuwauwa kigaidi makamanda hao wawili ambao walikuwa na mchango muhimu na athirifu katika vita dhidi ya ugaidi huko Syria na Iraq ilitolewa na rais wa wakati huo wa Marekani.

Nukta muhimu ni hii kuwa, kutolewa hukumu hii kunathibitisha kuwa vyombo vya mahakama vya Iraq bila ya kuathiriwa na mashinikizo ya Magharibi na bila ya kuhofia kukabiliwa na mashinikizo ya Marekani imemtaja waziwazi Donald Trump kuwa mtenda jinai na kutoa hukumu ya kumtia mbaroni. Kuhusiana na suala hilo, Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq amesema kuwa jukumu na kazi ya chombo cha mahakama cha Iraq katika kuwaadhibu wahusika wa mauaji ya makamanda wa ushindi ni maradufu; na kwamba chombo hicho hakitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayethibitika kuhusika katika jinai hiyo.

Kadhia nyingine muhimu ni kuwa, hukumu hii ya kutiwa mbaroni Trump imetolewa kwa kushirikiana viongozi wa Idara ya Mahakama ya Iran na wa Iraq. Ni wazi kuwa, maafisa wa vyombo vya mahakama vya nchi mbili za Iran na Iraq ndio waliofanya uchunguzi kuhusu watu waliohusika na jinai hiyo ya mauaji ya makamanda wa muqawama. Kazem Gharibabadi Naibu Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Idara ya Mahakama na Katibu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Iran hivi karibuni alibainisha kuwa raia 94 wa Marekani akiwemo Trump wanatuhumiwa kwa mauaji ya Shahidi Soleimani na wanajihadi wenzake. Kazem Gharibabadi aidha alisema kuwa, vyombo vya mahakama vya Iran na Iraq vinashirikiana kufuatilia jinai hiyo na kwamba miaka miwili iliyopita ziliundwa kamati za pamoja kati ya vyombo vya mahakama vya nchi mbili.  Wakati huo huo kamati hiyo ya pamoja imefanya duru tatu za vikao vyake huko Baghdad na hapa Tehran. Gharibabadi ameongeza kuwa, katika fremu ya kamati hiyo ya pamoja, pande mbili zimebadilishana taarifa na nyaraka nzuri sana’ ambapo taarifa zilizotolewa zimewasaidia maafisa wa vyombo vya mahakama vya nchi mbili ili kukamilisha zaidi uchunguzi wao.

Ushirikiano huu tajwa unaonyesha kuwa nchi mbili za Iran na Iraq ziko jadi na zina azma thabiti ya kufuatilia kisheria wahusika wa jinai ya mauaji ya makamanda wa muqawama; na tunaweza kuwa na matarajio ya kutolewa hivi karibuni hukumu za wahusika wengine.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *