Waislamu nchini Nigeria wamelaani kitendo cha dharau, kejeli na udhalilishaji cha jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha vibonzo vya kumvunjia heshima Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Mohammad Habib Abdullah, Katibu ya kundi la Waislamu Nigeria waliokerwa na uafiriti huo wa jarida la Kifaransa amesema katika kikao na waandishi wa habari katika jimbo la Bauchi kuwa, uchokozi huo wa jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo dhidi ya Uislamu na shakhsia wa dini hiyo tukufu unakusudia kuziumiza hisia za Waislamu kote duniani.
Amesema kitendo cha jarida hilo lenye sera za chuki dhidi ya Uislamu cha kuchapisha katuni za kumdhalilisha Kiongozi Muadhamu kinakusudia kuwahamakisha Waislamu kote duniani.
Amebainisha kuwa, hatua hiyo imejiri katika hali ambayo, madola ya Magharibi karibuni yalikula njama za kuchochea ghasia na fujo nchini Iran, na kuwahamasisha Wairani wasimame dhidi ya mfumo wa Kiislamu unaotawala hapa nchini.
Abdullah ameongeza kuwa, ni wazi kuwa jarida hilo haliwezi kuruhusiwa kukosoa uvamizi na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina licha ya kuwepo kwa ushahidi unaoonesha jitihada za kimfumo za utawala huo pandikizi za kuangamiza kizazi cha Wapalestina, na kuwafukuza kwenye maeneo na ardhi zao.
Katika toleo lake maalumu la Jumatano iliyopita ya Januari 4, jarida hilo la Ufaransa lilifanya kitendo cha kipuuzi cha kuanzisha shindano la kimataifa la michoro na vibonzo, ambapo lilichapisha picha za kuudhi zilizoandamana na maneno na misemo michafu na ya matusi dhidi ya Kiongozi Muadhamu.
Kufuatia hatua ya jarida la Ufaransa la Charlie Hebdo ya kukashifu na kuvunjia heshima wanazuoni, matukufu na thamani za kidini na kitaifa za Iran, balozi wa Ufaransa mjini Tehran aliitwa Jumatano katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ili kubainishiwa malalamiko ya Iran kuhusu kitendo hicho cha dharau.
Kabla ya hapo pia, Nasser Kan’ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, alisema Ufaransa haina haki ya kutusi matukufu ya nchi nyingine na hasa mataifa ya Kiislamu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.