Visa vya maambukizi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kipindupindu nchini Malawi vimezidi kuongezeka huku mikoa ya Tanzania inayopakana na nchi hiyo mikakati ikizidi kuimarishwa ili ugonjwa huo usiingie.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, idadi ya watu wanaopoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Malawi imezidi kuongezeka kutoka watu 661 hadi kufikia vifo 687.
Akizungumza na vyombo vya habari, Waziri wa Afya wa Malawi Khumbize Chiponda amesema, Januari 5 tayari kulikuwa na vifo 661 na kufikia Januari 7, watu 687 walikuuwa wamepoteza maisha kwa kipindupindu.
Malawi wiki iliyyopita iliahirisha kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari kwa angalau wiki mbili kutokana na mlipuko wa kipindupindu.
Muhula huo mpya ulipangwa kuanza Januari 3, lakini ongezeko la visa vya maambukizi ya kipindupindu na vifo vimeilazimu serikali kufuta mipango ya kufungua shule inapokabiliana na mlipuko huo.
Kipindupindu ni ugonjwa wa kuharisha unaosababishwa na kula chakula au kunywa maji yaliyo na bakteria aina ya Vibrio cholera, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema.
Kipindi cha kuibuka dalili za maradhi hayo ni kati ya saa 12 na siku tano baada ya kula chakula au kunywa maji machafu. Ugonjwa huo unasalia kuwa tishio la kimataifa kwa afya ya umma, lakini ni ugonjwa unaotibika.
Tayari Serikali ya Tanzania imetuma jopo la wataalamu 11 wakiwemo madaktari, watalaamu wa magonjwa ya mlipuko pamoja na maofisa afya mazingira katika mikoa Mbeya, Ruvuma na Songwe kudhibiti ugonjwa huo usiingie katika nchi hiyo.