Askari polisi nchini Ufaransa wamewashambulia vibaya maelfu ya watu walioshiriki maandamano ya Vizibao vya Njano, kulalamikia sera za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo na hususan mageuzi tata ya pensheni yanayotazamiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu wa 2023.
Polisi ya Ufaransa imewashambulia waandamanaji hao waliokuwa wamekusanyika katika medani ya Breteuil mjini Paris kwa mabomu ya gesi ya kutoa machozi na risasi za mipira. Makumi ya waandamanaji hao wamejeruhiwa, baadhi yao wakilazwa hospitalini kwa majeraha.
Hatua hizo za ukandamizaji wa polisi wa Ufaransa dhidi ya waandamanaji wanaopinga mfumo wa kibepari, zimekabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Mbali na kulalamikia mageuzi hayo ya sheria ya kustaafu, waandamanaji hao nchini Ufaransa wanalalamikia pia mfumko wa bei za bidhaa, mgogoro wa nishati, na ughali wa maisha uliotokana na mtikisiko wa uchumi wa nchi hiyo.
Wakati huo huo, ongezeko kubwa la mfumuko wa bei na gharama ya maisha nchini Ufaransa na kutokuwapo mlingano baina ya gharama za matumizi na mapato ya sehemu kubwa ya Wafaransa, kumesababisha wimbi la migomo katika nchi hiyo ya Ulaya.
Wafanyakazi nchini Ufaransa wanalalamikia ongezeko la umri wa kustaafu kutoka umri wa miaka 62 ya sasa hadi miaka 65 katika sheria hiyo tatanishi.
Serikali ya Macron hivi karibuni ilidokeza uwezekano wa kutazamwa upya mpango huo tata wa kubadilisha sheria za pensheni, hatua ambayo wadadisi wa mambo wanaona kuwa ni kusalimu amri mbele ya wapinzani wa mpango huo.