Wizara ya Ulinzi ya Russia imetangaza kuwa, wanajeshi 600 wa Ukraine wameangamizwa katika shambulio la makombora la ulipizaji kisasi la Moscow katika eneo la Donbass.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, shambulio hilo la jana Jumapili la makombora katika mji unaoshikiliwa na Kiev wa Kramatorsk katika eneo la Donbass ilikuwa ‘operesheni ya kulipiza kisasi’ dhidi ya jeshi la Ukraine.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imefafanua kuwa, Moscow imechukua hatua ya kulipiza kisasi kufuatia ‘shambulio la jinai’ la Kiev dhidi ya makazi ya muda ya askari wa Russia katika mji wa Makeyevka katika Jamhuri ya Watu wa Donetsk usiku wa kuamkia mwaka mpya (2023).
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, askari 89 wa nchi hiyo waliuawa katika shambulio hilo la Ukraine kwa kutumia makombora sita ya Marekani ya HIMARS usiku wa kuamkia Januari Mosi, 2023.
Hivi karibuni, Rais wa Russia, Vladimir Putin alisisitiza kuwa, Moscow haitaziruhusu nchi za Magharibi kuwatumia watu wa Ukraine kwa ajili ya kuigawa na kuidhoofisha Russia.
Haya yanajiri siku chache baada ya Marekani kutangaza kuiongezea Ukraine msaada wa kijeshi wa dola bilioni 1.85 ikiwa ni pamoja na kuipelekea Ukraine mfumo wa makombora wa Patriot.