Fedheha! Uingereza yashindwa kutuma satalaiti yake anga za mbali

Jaribio la Uingereza la kuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kurusha satalaiti katika anga za mbali limegonga mwamba, huku kampuni ya Virgin Orbit ikitangaza kuwa roketi lake la kurushia satalaiti hiyo lilikubwa na hitilafu na kuifanya (satalaiti hiyo) ishindwe kufika katika anga za mbali.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, roketi la LauncherOne la kampuni ya Virgin Orbit limekubwa na mushkili na kushindwa kuiweka satalaiti hiyo iliyopewa jina la “Cosmic Girl” katika anga za mbali. Uzinduzi huo uliofeli umefanyika mapema Jumanne katika mji wa pwani wa Newquay, kusini magharibi mwa Uingereza.

Awali shirika la Virgin Orbit lilitangaza katika ukurasa wake wa Twitter kuwa roketi la LauncherOne limefika katika anga za mbali, lakini baadaye ikalazimika kuufuta ujumbe huo baada ya jaribio hilo kufeli na roketi hilo kudondoka katika Bahari ya Atlantic.

Hili ni pigo la pili kwa Ulaya, baada ya roketi la Vega-C lililoundiwa Italia kufeli tena katika uzinduzi mwingine ulioshia kwa fedheha katika eneo la Guiana la Ufaransa, mnamo Disemba mwaka uliomalizika.

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, mwishoni mwaka uliomalizika, Magharibi ilighadhabishwa na hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kurusha satalaiti katika anga za mbali kwa mafanikio, kwa kutumia roketi la Russia. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema katika taarifa kuwa, kitendo cha Russia cha kupanua uhusiano na ushirikiano na Iran kinapaswa kutazamwa na dunia kama tishio kubwa.

Maafisa wa Marekani wametiwa kiwewe na mafanikio hayo makubwa ya Iran katika teknlojia ya anga za mbali, licha ya kuwekewa vikwazo vikali na kuwa chini ya mashinikizo ya juu kabisa ya Washington.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *