Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa umoja huo unajaribu kila linalowezekana kuondoa vizuizi vinavyokwamishwa usafirishaji wa mbolea ya Russia.
Stephane Dujarric Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuhusu kusafirishwa mbolea ya Russia kufuatia vita vinavyoendelea huko Ukraine kwamba, Katibu Mkuu Antonio Guterres na viongozi wengine wa umoja huo wanaendelea kufanya juhudi ili kuondoa vizuizi na masuala yote yanayokwamisha usafirishaji wa nafaka na mblea kutoka Russia.
Uturuki, Umoja wa Mataifa, Russia na Ukraine Julai 22 mwaka jana zilisaini makubaliano huko Istanbul kwa ajili ya kuanza tena kusafirishwa nafaka na mbolea kutoka Ukraine na Russia kufuatia kujiri vita kati ya nchi mbili hizo.
Viongozi wa Ukraine wameeleza kuwa hadi sasa meli 580 zilizopakia tani milioni 15 za nafaka zimeondoka katika bandari za UKraine tangu kutiwa saini makubaliano hayo ya Istanbul.
Marekani na nchi kadhaa za Magharibi zimeiwekea Moscow vikwazo vikubwa kufuatia oparesheni za kijeshi zilizoanzishwa na Russia dhidi ya Ukraine mnamo Februari 24 mwaka jana.