Vigogo wa upinzani kurejea Tanzania kufuatia tangazo la Rais Samia

Huku Chama cha Demokrasia ya Maendeleo ‘Chadema’ kikitarajia kuzindua mikutano ya hadhara Januari 21 mwaka huu nchini Tanzania, viongozi wa chama hicho kikuu cha upizani walioko nje ya nchi, Tundu Lissu, Godbless Lema na Ezekia Wenje wanatazamiwa kuwa miongoni mwa washiriki katika mikutano hiyo.

Mikutano ya hadhara ya chama hicho inatarajiwa kuanza baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, mbele ya viongozi wa vyama 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, kutangaza Januari 3 mwaka huu kuondoa zuio lililokuwepo.

Zuio hilo liliwekwa mwaka 2016 na Rais wa wakati huo, John Magufuli akitaka mikutano hiyo ihusishe wabunge na madiwani pekee waliochaguliwa, huku wengine wakitakiwa kufanya mikutano ya ndani ambayo nayo wakati mwingine ilikuwa inazuiwa.

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho-Bara, yupo Ubelgiji na Lema, mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, anaishi Canada huku Wenje akiwa nchini Marekani; na wote kwa pamoja waliondoka nchini wakihofia usalama wao baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Katika uchaguzi huo, Lissu alikuwa mgombea urais akichuana na mgombea wa CCM, Magufuli àmbaye aliibuka mshindi huku Lema akishindwa kutetea ubunge wa Arusha Mjini dhidi ya Mrisho Gambo wa CCM.

Gazeti la Mwananchi limeandika kuwa, taarifa za Lissu na Lema kurejea nchini zimedokezwa na chanzo cha gazeti hilo ndani ya kamati kuu ya Chadema iliyoketi hivi karibuni, kuwa Lissu na Lema watakuwa nchini kabla ya Januari 21, mwaka huu.

Chanzo hicho kilisema kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika kupitia mtandao Januari 5 kupokea taarifa ya maridhiano baina ya CCM, Serikali na Chadena pamoja na mambo mengine, kiliazimia wanasiasa hao warejee nchini.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema kina Lissu waliondoka wakiwa na sababu za msingi, hivyo hata kurejea nchini lazima wajiridhishe kama mazingira ni salama. Amesema, “Kama chama tungetamani wote tuwepo tuijenge Chadema ili tujiandae na 2025, haya ndiyo matamanio ya chama na ushauri ni kwamba kama wanaweza kurejea warejee.”

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *