Watu wasiopungua wanne wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga bomu katika shambulio linaloshukiwa kufanywa na genge la ukufurishaji la al Shabab, huko Garisa, kaskazini mwa Kenya.
Jeshi la Polisi laa Kenya limethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Wahandisi wa Mamlaka ya Taifa ya Barabara za Kenya ni miongoni mwa watu waliouawa kwenye shambulizi hilo la kigaidi.
Polisi wamesema, gari waliyokuwa wakisaifiria watu hao ilikanyaga bomu lililotegwa kando ya barabara na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi na kuua watu wanne wakiwemo wahandisi watatu wa Mamlaka ya Barabara Kuu ya Kenya (KeNHA) waliokuwa kwenye zoezi la kawaida la kutathmini barabara za eneo hilo.
Sehemu nyingine ya taarifa ya polisi imesema, gari hiyo ilikuwa ni sehemu ya msafara uliolazimika kurudi nyuma baada ya gari la Toyota Hilux Double Cabin kuharibiwa kwenye shambulio hilo.
“Magari mengine yalirudi kwenye kambi ya Wachina ya Hailey,” imesema sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya polisi.
Mkuu wa polisi wa kanda ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya, George Seda amesema kuwa, washambuliaji walikimbia na polisi wametumwa katika eneo hilo kuwasaka na kuimarisha usalama.
Maeneo hayo ya Kaunti ya Garissa ndiyo yaliyoshuhudia shambulio kama hilo lililoua maafisa wawili wa polisi na raia mmoja mwezi Disemba.
Shambulio hilo lilihusishwa na magaidi wa al Shabab walioingia Kenya kupitia mpaka wa Somalia na kufanya mashambulizi.