Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China ametoa mwito kwa bara la Afrika kupatiwa kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Qin Gang amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo mjini Addis Ababab Ethiopia na Moussa Faki Mahamati, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika na kusisitiza kwamba, Afrika lazima iwe na sauti kubwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa.
Aidha ameongeza kuwa, kuna haja ya kuweko mfumo wa haki na usawa zaidi wa utawala wa kimataifa” akibainisha kwamba, Afrika inapaswa kuwa njia panda ya ushirikiano wa kimataifa, sio msingi wa ushindani mkubwa wa mamlaka”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Moussa Mahamat Faki amesema sio haki kuliona bara la Afrika halina kiti cha kudumu katika baraza kuu la dunia.
“Kwa miongo kadhaa sasa tumekuwa tukipambana kwa ajili ya mageuzi ya mfumo wa kimataifa kwa ujumla na hasa kwa niaba ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,” alisema.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaundwa na wanachama 15, wakiwemo wanachama watano wa kudumu wenye haki ya kura ya turufu ambao ni Marekani, Russia, China, Ufaransa na Uingereza. Nchi nyingine kumi zinakalia viti vingine viisivyo vya kudumu kwa muda wa miaka miwili.
Viongozi wa Afrika na hata wa mataifa mengine kama China yamekuwa yakikosoa muundo huo wa Baraza la Usalama ambao unaikandamiza na kuidhulumu Afrika yenye mataifa mengi na idadi kubwa ya watu.’