Serikali ya Rwanda imesema kwamba haina nia wala azma yoyote ya kuwafukuza au kuwapiga marufuku kuingia nchini humo wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Msemaji wa serikali ya Rwanda, Yolande Makolo amekanusha uvumi ulioenezwa kwenye vyombo vya habari kuwa Rais Paul Kagame amtaka wakimbizi wa Kongo warejee nchini kwao na kusema kuwa vyombo vya habari vilitafsiri vibaya matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Paul Kagame kwamba Rwanda haiwezi kuendelea kuwapokea wakimbizi wa Kongo.
Katika sehemu moja ya matamshi yake, Bi Yolande Makolo amesema: “Nchi ya milima elfu bado inakaribisha watu wanaokimbia ukosefu wa usalama, mateso na vurugu. Tunatoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua jukumu la kutafuta suluhu la kudumu kwa kundi hili la wakimbizi waliosahaulika kutoka DRC.”
Matamshi ya Kagame, ambayo aliyatoa bungeni hivi karibuni, yamezua hisia hasi, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Shirika la kimataifa la Human Rights Watch (HRW) lilisema: “Tamko la Rais Kagame linaonyesha kwa uwazi hatua ya serikali ya Rwanda ya kuingiza siasa katika suala la haki za wakimbizi. Matamshi hayo ya Rais Kagame yamekuja wakati huu ambapo Rwanda ndiyo kwanza imefikia makubaliano yasiyo ya kiuaminifu ya dola milioni 145 na Uingereza ya kuchukua waomba hifadhi ya ukimbizi wanaowasili Uingereza kupitia njia zisizo za kawaida.”
Uhusiano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda umefikia hatua ya chini kabisa huku uongozi nchini DRC ukiishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23. Rwanda inakanusha kuwaunga mkono waasi hao.
Mapigano yanaendelea hivi sasa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23, ambao wameteka maeneo mengi ya mashariki mwa nchi hiyo.