Katibu Mkuu wa UN: Tunalaani mauaji na hatua zote zisizo halali za Israel dhidi ya Wapalestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu matokeo hasi na yenye madhara kwa upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, Antonio Guterres amesisitiza kuwa, hatua za Israel za kupanua vitongoji vya walowezi, kubomoa nyumba za Wapalestina na kuhawamisha kwa nguvu katika makazi yao zinashadidisha ghadhabu na hali ya kukata tamaa kwa wananchi hao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kwa kusema, “mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa maafa makubwa ya vifo kwa Wapalestina. Tunalaani mauaji na vitendo vyote visivyo halali vya Israel”.
Aidha Guterres amesema: “ningali nina wasiwasi mkubwa kutokana na hatua za upande mmoja tulizoshuhudia katika siku za karibuni zilizochukuliwa na viongozi wa Israel dhidi ya Wapalestina”.

Katika upande mwingine, Rashidah Tlaib, mbunge wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani mwenye asili ya Palestina ameeleza katika ujumbe wa Twitter alioandika hivi karibuni kwamba, 2022 ulikuwa moja ya mwaka wa mauaji makubwa zaidi ya Wapalestina na akasisitiza kuwa Baraza la Wawakilishi la Marekani linapaswa kukomesha misaada ya kifedha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tlaib amebainisha katika ujumbe wako huo kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina yamepelekea kuuawa shahidi Wapalestina zaidi ya 200 wakiwemo watoto zaidi ya 50, kujeruhiwa maelfu ya wengine na kubomolewa zaidi ya nyumba 800 za Wapalestina.
Kabla ya hayo, Ofisi ya Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ilieleza katika ripoti yake ya hivi karibuni, kwamba 2022 ulikuwa mwaka mkubwa zaidi wa kumwagwa damu za Wapalestina tangu 2005, ambapo katika mwaka huo watu 230 waliuawa kwa kupigwa risasi na Wazayuni.
Ili kufikia malengo yao ya kujipanua, askari wa utawala haramu wa Israel na walowezi wa Kizayuni wanavamia na kushambulia kila siku maeneo tofauti ya Palestina na kuwaua shahidi, kuwajeruhi au kuwatia nguvuni Wapalestina wasio na hatia.
Kutokana na jinai na udhalimu huo unaofanywa na Wazayuni, wanamapambano wa Kipalestina wanatumia kila njia na nyenzo walizonazo kujibu jinai hizo zisizohesabika.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *