Muungano vamizi wa Saudia waendelea kukiuka usitishaji vita nchini Yemen

Muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umeendelea kukiuka makubaliano ya usitishaji viita ambapo katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita umekiuka usitishaji vita huo zaidi ya mara 140.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita, majeshi ya muungano vamizi wa Saudia yameshambulia kwa makombora mji wa bandari wa al-Hudaydah zaidi ya mara 140 na kusababisha uharibifu mkubwa.

Pamoja na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kuafiki makubaliano ya usitishaji vita lakini umekuwa ukiyakiuka mara kwa mara na hivyo kudhihirisha wazi kwamba, hauna nia ya dhati ya kutekeleza usitishaji vita nchini Yemen.

Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amewahi kueleza bayana kwamba, usitishaji vita nchini Yemen ulisharambatika na haupo kutokana na majeshi ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia kukiuka mara kwa mara usitishaji vita huo.

Saudi Arabia huku ikungwa mkono na Marekani na nchi nyingine kadhaa, Machi 25 mwaka 2015 zilianzisha hujuma na mashambulizi makubwa huko Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, angani na nchi kavu.

Vita hivyo vya kidhulma vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen hadi sasa vimesababisha kuuliwa maelfu ya Wayemeni, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine.

Aidha asasi na jumuiya mbalimbali za misaada ya kibinadamu zimetahadharisha mara chungu nzima kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Yemen na hata uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *