Magaidi wakufurishaji waua Waislamu tisa ndani ya msikiti kaskazini-mashariki ya Burkina Faso

Watu tisa wameuawa wakati watu wanaoshukiwa kuwa magaidi wakufurishaji wenye misimamo ya kufurutu ada waliposhambulia msikiti mmoja kaskazini mashariki mwa Burkina Faso.

Duru za habari zimemnukuu shuhuda mmoja akisema, shambulio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatano katika kijiji cha Goulgountou katika eneo la Sahel nchini Burkina Faso, wakati washambuliaji walipofika kwa pikipiki kijijini hapo na kuwakusanya waumini ndani ya msikiti huo.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakufurishaji hao waliwatenganisha wanawake, watoto na wazee kisha wakatoa mahubiri ya kuwashawishi waumini msikitini humo waachane na itikadi za kidini walizonazo.

Shuhuda huyo amesema, majadiliano yalianza baina yao na Imamu, na kwa sababu Imamu huyo hakukubaliana nao walimuua.

“Walijaribu kumkata koo, lakini alijitetea, akisema alitaka kufa akiwa amesimama wima, hivyo magaidi walimpiga risasi kichwani,” ameeleza mkazi huyo wa kijiji cha Goulgountou, akiongeza kuwa alihudhuria mazishi ya waliouawa jana Alkhamisi.

Aidha amesema, waumini wengine wanane, hasa viongozi wa jamii ya wanakijiji, waliuawa kwa kupigwa risasi kwa sura hiyo hiyo.”

Kijiji cha Goulgountou kiko karibu na mji wa uchimbaji dhahabu wa Falagountou, ambao uko karibu na mpaka wa pamoja wa Burkina Faso na Niger.

Ripoti kutoka kijiji hicho zinaeleza kuwa, tangu mwanzoni mwa wiki hii, eneo hilo limekumbwa na uvamizi mara kadhaa wa watu wanaoshukiwa kuwa wakufurishaji wenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu magaidi hao wakufurishaji waanze kuishambulia Burkina Faso kutokea nchi jirani ya Mali mnamo 2015.

Zaidi ya theluthi moja ya eneo la nchi hiyo liko nje ya udhibiti wa serikali.

Hujuma na mashambulio ndani ya ardhi ya Burkina Faso yamechochea kuzuka mapinduzi mawili mwaka jana yaliyofanywa na maafisa wa jeshi waliokasirishwa na kuongezeka idadi ya raia wanaouawa katika mashambulio hayo.

Utawala wa kijeshi wa sasa wa Burkina Faso unaongozwa na Kapteni Ibrahim Traore, ambaye akiwa na miaka 34 ndiye kiongozi mwenye umri mdogo zaidi duniani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *