Maonyo makali ya kimataifa yametolewa kuhusu ukame mkali unaotokana na kushadidi baridi na kuongezeka mgogoro wa kiuchumi nchini Afghanistan. Jamii ya kimataifa inasisitiza kuwa, iwapo hali ya hivi sasa itaendelea, basi wananchi milioni 6 wa Afghanistan watakumbwa na ukame wa kuchupa mipaka.
Jan Egeland, Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway ambaye hhivi karibuni alitembelea Kabul, mji mkuu wa Afghanistan ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, iwapo wanawake wataendelea kupigwa marufuku kufanya kazi katika taasisi zisizo za kiserikali huko Afghanistan, basi Waafghani wasiopungua milioni 6 watatumbukia kwenye ukata mkubwa. Mkuu huyo wa baraza la masuala ya wakimbizi la Norway vile vile amesema, iwapo hali ya hivi sasa itaendelea, watoto laki sita wa Afghanistan watakosa masomo, watu milioni 13 watakosa maji safi ya kunywa na milioni nne wengine watakosa huduma za lazima za afya na matibabu.
Jan Egeland ambaye alitembelea Afghanistan siku ya Jumatano, amewataka viongozi wa serikali ya Taliban kuruhusu wanawake wafanye kazi. Lililo muhimu zaidi kuzingatiwa hapa ni kwamba katika kipindi cha miongo minne ya mapigano ya ndani na kukaliwa kwa mabavu Afghanistan, wanawake wengi sana wamepoteza waume zao na mamilioni ya watoto wa Afghanistan ni mayatima. Unapozingatia hayo utaona kuwa, waendeshaji wakubwa wa familia za Afghanistan ni mama ambao wamepoteza waume zao na wanaendesha familia hizo katika mazingira magumu mno ya nchi iliyosambatishwa na vita vya makumi ya miaka. Bila ya hata kufikiri sana, mtu anaweza kuelewa kuwa mamia ya maelfu ya familia za Afghanistan hivi sasa zina matatizo chungu nzima ya ukosefu wa chakula na mahitaji ya lazima.
Hosseini Mazari ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya Afghanistan. Anasema: Badala ya wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC au wa nchi za Waislamu kwenda Kabul kuzungumza na viongozi wa Taliban, tunaona viongozi wa nchi za Ulaya na Magharibi ndio wanaokwenda huko kufanya mazungumzo na Taliban. Hili linathibitisha jinsi masuala ya kidiplomasia yalivyo dhaifu sana katika nchi za Waislamu na jinsi jumuiya kama ya OIC isivyoguswa na masuala muhimu ya Ulimwengu wa Kiislamu. Hivi sasa roho za mamia ya maelfu ya Waislamu na wananchi wa Afghanistan ziko hatarini, lakini huoni viongozi wa nchi na taasisi za Waislamu zikilipa umuhimu suala la angalau kwenda kuzungumza na viongozi wa Taliban ili kuwaokoa Waislamu hao.
Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba, msababishaji mkuu wa matatizo na migogoro isiyo na idadi ya Afghanistan ni jinai za miaka mingi za wanajeshi vamizi wa Marekani na Uingereza. Hivi sasa pia Marekani inashikilia karibu dola bilioni 10 za mali za wananchi wa Afghanistan kwa visingizio chapwa na bila ya kujali masaibu na matatizo makubwa waliyo nayo wananchi wa kawaida huko Afghanistan. Mashirika ya nchi za Ulaya na ya Magharibi yanayodai kupigania haki za binadamu, yanafumbia macho jinai zote hizo za nchi za kiistikbari hasa Marekani na Uingereza na hayaguswi na masaibu ya wananchi wa Afghanistan. Miaka mingi ya jinai za Marekani na Uingereza imewazuia wananchi wa Afghanistan kufanya kazi zao za lazima hasa kilimo na hiyo ni miongoni mwa sababu kubwa za kushadidi njaa na ukata nchini humo. Sasa hivi Afghanistan inashindwa hata kujidhainia mahitaji yake ya lazima yakiwemo ya kilimo huko Marekani ikiendelea kuzuia mali za dola bilioni 10 za wananchi wa Afghanistan, zisitumike kuwaondolea matatizo wananchi hao.
Amin Farjad, mtaalamu mwingine wa masuala ya Afghanistan anasema: Afghanistan ina kiwango cha kutosha cha maji ya kuweza kutumika kwa ajili ya kilimo. Lakini inasikitisha kuona kuwa neema hiyo haukutumika vizuri kwenye miaka ya huko nyuma na sasa hivi wananchi wa Afghanistan wanateseka kwa njaa na ukame. Wavamizi wa Afghanistan walizuia hata kutekelezwa mradi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kutumia kilimo kama sehemu muhimu ya kuwadhaminia mahitaji ya lazima ya chakula, wananchi wa Afghanistan.
Kiujumla ni kwamba kuna mambo mengi yanayopelekea wananchi wa Afghanistan waendelee kuteseka. Mionogni mwake ni matatizo yaliyosababishwa na jinai za nchi za Magharibi hasa Marekani na Uingereza na pia siasa za serikali ya kundi la Taliban kama za kuzuia wanawake wasifanye kazi, wakati uhakika unaonesha kuwa familia nyingi sana za Afghanistan zimepoteza wazazi wa kiume katika miaka mingi ya mapigano ya ndani.