Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran itaendelea kushirikiana na serikali halali ya Syria.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo leo mjini Damascus mji mkuu wa Syria katika mazungumzo yake na Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad na kusisitiza kwamba, himaya ya Tehran kwa serikali ya Syria katika kipindi chote cha mgogoro na msaada wake kwa nchi hiyo katika kupambana na makundi mbalimbali ya kigaidi ni ushahidi na ithbati ya taifa hili kushirikiana na nchi hiyo ya Kiarabu.
Mazungumzo ya Dakta Abdollahian na Rais Bashar al-Assad yalijikita zaidi katika masuala ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto zinazoyakabili mataifa hayya rafiki.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alielekea Syria akitokea Beiuri Lebanon ambapo akiwa nchini humo alikutana na kuzungumza na Sayyid Hassan Nasrallah” Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.
Amir-Abdollahian alisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuunga mkono kwa dhati wananchi, serikali, jeshi na harakati ya Hizbullah ya Lebanon.
Aidha akiwa nchini Lebanon alisema, Iran inatoa wito kwa mirengo yote ya kisiasa ya Lebanon kuendelea na mazungumzo na makubaliano kuelekea uchaguzi wa rais na kukamilika kwa mchakato wa kisiasa.
Kuhusiana na mkwamo wa kuchaguua Rais, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa: Mirengo tofauti ya kisiasa nchini Lebanon ndiyo itakayoamua rais mpya wa nchi hiyo kwa umahiri na bila ya uingiliaji wowote wa kigeni.