Watu wasiopungua 44 wamefariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imebeba watu 72 kuanguka nchini Nepal.
Ndege hiyo imeanguka mapema leo ilipokuwa ikisafiri kutoka mji mkuu Kathmandu kuelekea Pokhara . Pokhara ni mji wa kitalii wenye shughuli nyingi na uko karibu kilomita 200 (maili 124) magharibi mwa Kathmandu.
Sudarshan Bartaula, msemaji wa shirika la ndege la Yeti linalomiliki ndege hiyo amesema, watu 72 wakiwemo wahudumu wanne walikuwemo ndani ya ndege hiyo aina ya ANC ATR72.
Msemaji wa polisi ya Nepal Tek Prasad Rai amevieleza vyombo vya habari kuwa, idadi ya vifo imefika 44 na kwamba hadi sasa hakuna manusura aliyepatikana katika ajali hiyo.
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Nepal Jagannath Niroula amethibitisha idadi hiyo ya vifo akifafanua kuwa, maiti 30 tayari zimepatikana na kuhamishiwa hospitalini na utaratibu ulikuwa unafanywa kuzihamisha zingine 14 katika eneo ilipoangukia ndege hiyo.
Ameongeza kuwa ajali hiyo ndio mbaya zaidi kutokea nchini humo tangu ile ya Machi 2018 iliyoua watu 51 kati ya 71 waliokuwemo ndani ya ndege ya shirika la ndege la US-Bangla.
Kwa mujibu wa taarifa ya mamlaka hiyo, ndege hiyo iliwasiliana na uwanja wa ndege kutokea Seti Gorg saa nne na dakika 50 asubuhi kisha ikaanguka.
Wakazi wa eneo ilipoangukia ndege hiyo wamesema, hali ya hewa ilikuwa nzuri na anga ilikuwa safi kiasi cha kuwafanya washtushwe na kushangazwa na ajali hiyo. Hata hivyo mashuhuda wamesema, ndege hiyo ilionyesha kuwa na hitilafu kabla ya kuanguka karibu na uwanja wa ndege.
Hata hivyo hadi sasa chanzo halisi cha ajali hiyo bado hakijajulikana.