Mripuko mbaya zaidi wa kipindupindu waikumba Malawi, umeshaua watu 750

Idadi ya vifo katika mripuko mbaya zaidi wa kipindupindu kukwahi kuikumba Malawi katika miongo miwili iliyopita, vimefikia 750.

Waziri wa Afya wa Malawi, Khumbize Kandodo Chiponda ametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, kwa sasa kuna wagonjwa 892 hospitalini, wakati kesi zikiendelea kuripotiwa katika wilaya 27 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Nchi ya Malawi yenye takriban watu milioni 20 imerekodi kesi 22,759 za ugonjwa wa kipindupindu tangu kesi ya kwanza kabisa kukripotiwa mwezi Machi mwaka jana 2022.

Licha ya kuzuka mgogoro huo, lakini serikali imeamua kufungua tena skuli katika kitovu cha kibiashara cha Blantyre na mji mkuu Lilongwe kuanzia tarehe 17 mwezi huu wa Januari.

Awali skuli za Malawi zilipangwa kufunguliwa tena tarehe 3 Januari lakini zoezi hilo limeakhirishwa kwa wiki mbili.

Waziri Chiponda amesema, Wizara ya Afya ya Malawi imeridhishwa na hatua za usafi na hali jumla ya miji ya Blantyre na Lilongwe ambayo ina zaidi ya watu milioni 2.

Kipindupindu, ugonjwa wa kuharisha papo kwa papo na unaweza kusababisha upungufu mkubwa wa maji mwilini na kifo ikiwa hautawahi kutibiwa.Dk. Gama Bandawe wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Malawi amesema kuwa, ugonjwa wa kipindupindu nchini humo unazidi kudhibitiwa na idadi ya vifo inabidi ianze kupungua.

Serikali ya nchi jirani ya Tanzania imetuma jopo la wataalamu wakiwemo madaktari, watalaamu wa magonjwa ya mripuko pamoja na maafisa afya mazingira katika mikoa Mbeya, Ruvuma na Songwe iliyoko karibu na Malawi katika juhudi za kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini humo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *