Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zimbabwe zimeazimia kupanua zaidi ushirikiano wao katikka nyanja mbalimbalii ukiwemo uga wa michezo.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha tisa cha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na taifa la Kiafrika la Zimbabwe kilichofanyika leo hapa mjini Tehran.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, imependekezwa katika kikao hicho cha pande mbili kilichofanyika katika makao ya Wizara ya Ushirikiano, Kazi na Ustawi wa Jamii ya Iran kwamba, mbali na masuala ya kisiasa Iran na Zimbabwe ziwe na ushirikiano mpana pia katika uga wa michezo.
Mwakilishi wa Wizara ya Michezo na Vijana mbali na kutoa ripoti kuhusiana na nyaraka za karibuni kabisa za ushirikiano bnaina ya pande mbili amesema, kuna haja ya kupanuliwa zaidi ushirikiano wa kimichezo baina ya mataifa haya mawili.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa kipaumbele katika sera zake za kigeni juu ya suala la kuwa na uhusiano na ushirikiano sambamba na kuimarisha uhusiano na mataifa ya Kiafrika na hilo limekuwa likitiwa mkazo mno na serikali ya sasa ya awamu ya 13 inayoongozwa na Rais Ebrahim Raisi.
Zimbabwe ni miongoni mwa mataifa ya Kiafrika ambayo kwa miaka mingi sasa imekuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.