Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imeilaani vikali Marekani kwa kulenga sekta ya afya ya nchi hiyo ya Kiarabu kwa vikwazo vya upande mmoja.
Katika taarifa, wizara hiyo imetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kusimamisha vikwazo hivyo vya kikatili vya Marekani dhidi ya sekta ya afya ya taifa hilo la Kiarabu.
Damascus imebainisha kuwa, vikwazo hivyo vipya vya Marekani vilivyolenga sekta ya afya ya Syria ni muendelezo wa hatua za kikatili za Washington dhidi ya taifa hilo ambalo liko chini ya mzingiro.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imefafanua kuwa, vikwazo hivyo vilivyotangazwa na Idara ya Viwanda na Usalama ya Marekani (BIS) vimezuia uagizaji wa vifaa na suhula za tiba zinazohitaji katika hospitali za umma na binafsi za nchi hiyo.
Imesema vikwazo hivyo, pamoja na taasisi na vituo vingine vya afya vya Syria, vimeilenga Hospitali ya Watoto iliyoko mjini Damascus, inayotoa huduma za afya kwa mamilioni ya Wasyria.
Mapema mwezi huu, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa alisema, Wamagharibi wanabeba dhima ya kushtadi hali mbaya ya kibinadamu nchini Syria kutokana na vikwazo vyao vya upande mmoja.
Vasily Nebenzya alisema kupuuza mateso wanayopata Wasyria kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani na EU kuna madhara na maafa makubwa kwa maisha ya kila siku ya raia, na hakuwaruhusu kupata huduma muhimu na za dharura kama gesi na umeme, hasa wakati huu wa msimu wa baridi kali.