Ukurasa mwingine wa maafa ya binadamu huko Yemen; wagonjwa elfu tano wanaohitaji huduma ya Dialysis wanakaribia kuaga dunia

Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen Anayehusika na Masula ya Tiba ameeleza kuwa maisha ya wagonjwa elfu tano wenye matatizo ya figo wako kwenye hatari ya kifo na Umoja wa mataifa na jamii ya kimataifa ndizo zinazopaswa kubeba dhima ya uhai na maisha ya raia hao wa Yemen.

Ali Jahaf Naibu Waziri wa Afya wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen Anayehusika na Masuala ya Tiba ameashiria kusalia tupu stoo za dawa zinazotumika kutolea huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa maradhi ya figo (Dialysis) na kutahadharisha kuwa Yemen inakaribia kupatwa na maafa ya binadamu yenye kutishia maisha ya wagonjwa elfu tano wanaosumbuliwa na matatizo ya kushindwa kufanya kazi figo.

Dakta Anis Al-Asbahi Msemaji wa Wizara ya Afya ya Yemen pia amesisitiza kuhusu nafasi na namna taasisi za kimataifa zinavyopasa kuwajibika katika kuokoa maisha ya wagonjwa wa figo nchini humo na kutaka kufunguliwa uwanja wa ndege wa Sana’a na bandari ya al Hudaydah ambazo ni njia kuu za kuingizia dawa na chakula kwa ajili ya mamilioni ya Wayemen.

Huko nyuma pia, Wizara ya Afya ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ilidokeza kuhusu upungufu wa dawa muhimu kufuatia kuendelea mzingiro wa muungano vamizi wa Saudia dhidi ya nchi hiyo na kutangaza kuwa upungufu wa damu unatishia maisha ya wagonjwa 40 wenye maradhi ya Thalassemia.

Wakati huo huo, tatizo la mafuta pia limeongezeka sambamba na kuanza kwa msimu wa baridi kali na licha ya duru za habari kuripoti kuwa watoto wameathiriwa na baridi kali katika kambi mbalimbali za wakimbizi huko Yemen. Huduma za matibabu zimesitishwa pia katika hospitali mbalimbali kutokana na ukosefu wa mafuta na umeme; hali ambayo inazidisha kasi ya vifo vya wagonjwa na hasa watoto wadogo.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa, zaidi ya watu milioni 23.4 yaani karibu robo tatu ya jamii nzima ya wananchi wa Yemen wakiwemo watoto milioni 12 na laki 9 wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu. Wakati huo huo watoto wa Yemen karibu milioni 2 na laki 2 wanasumbuliwa na utapiamlo mkali. Kuhusiana na hilo, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limetangaza kuwa watoto wa Kiyemeni 540,000 walio na umri chini ya miaka mitano wana utapiamlo mkali huku Wayemeni zaidi ya milioni 17.8 wakiwemo watoto wadogo milioni 9.2 pia wakiwa hawana maji safi na salama wala huduma za matibabu.

Shirika la Save The Children pia Disemba 29 mwaka jana lilitangaza kuwa Yemen inashika nafasi ya pili katika orodha ya nchi 8 zinazokabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula; na kwamba watu wenye utapiamlo mkali katika kipindi cha miaka miwili iliyopita huko Yemen wameongezeka na kufikia asilimia 66 yaani wameongezka kutoka milioni 3.6 hadi milioni 6.  Katika upande mwingine, kwa mujibu wa takwimu za karibuni za Umoja wa Mataifa, watoto elfu 11 wa Yemen  wamekuwa wahanga wa vita nchini kwao tokea mwaka 2015 hadi sasa na wengine zaidi ya 3700 pia wameaga dunia yaani kila siku watoto 4 huwa wahanga wa vita vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia huko Yemen.

Vita dhidi ya Yemen vilivyoanza mwaka 2015 kwa uvamizi wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia vimesababisha kujitokeza moja ya migogoro mikubwa zaidi ya haki za binadamu duniani. Hivi sasa Yemen inakabiliwa na changamoto kuu ya haki za binadamu ikiwemo kuzingirwa kiuchumi nchi hiyo na Saudi Arabia na kujiri njaa, kubomolewa vituo vya afya na hospitali na ndege za kivita za muungano vamizi wa Saudia, kuibuka magonjwa mbalimbali ya miripuko na ya kuambukiza, kubomolewa shule na vituo vya elimu na kushindwa watoto wa Yemen kwenda shule, kutiwa nguvuni wanaharakati wa vyombo vya habari na kuteswa na vibaraka wanaoungwa mkono na Imarati, vikosi vya Saudia na Imarati kuwatia nguvuni bila sababu wanaharakati wa kisiasa na kuwafunga katika jela zilizo chini ya ardhi, kudhalilishwa kijinsia wanawake na mabinti wa Yemen waliolazimika kuwa wakimbizi, wafanya magendo ya binadamu na mamluki wa Imarati kuwatia nguvuni wahajiri wa Kiafrika na kuwabaka.

Hakuna shaka kuwa, yale yanayofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudia kwa kushirikiana na Imarati yakijumuisha jinai mbalimbali, kwa upande mmoja, ni kutekelezwa jinai dhidi ya binadamu kwa kuzingatia ukubwa wake bila kujali uhalifu huo unatekelezwa dhidi ya mwanamke, mwanaume, mtoto, mwanajeshi au kwa raia wa kawaida. Katika upande mwingine, kwa kuzingatia kuwa vitendo vyote hivi vinatekelezwa dhidi ya wafuasi wa madhehebu maalumu na katika mazingira mabaya zaidi, ni wazi kuwa vinaweza kuhesabiwa kuwa ni mauaji ya halaiki ambayo ni katika jinai kubwa za kimataifa. Si hayo tu, bali vitendo vyote hivyo vinahesabiwa kuwa jinai za kivita kwa sababu vimetekelezwa katika vita vya kimataifa ambapo aghalabu ya jinai hizo kwa mfano mashambulizi dhidi ya makazi ya raia  na kuikalia kwa mabavu nchi ambayo ina mamlaka ya kujitawala, ni mojawapo ya mifano ya  wazi ya uhalifu wa kivita. Kesi zote hizi zinaweza kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria; na inaonekana kuwa  Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen italiweka suala hilo katika ajenda yake ya kazi iwapo haitaafikiana na Saudi Arabia kukomesha uvamizi na kulipwa fidia.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *