Ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na Russia unaenda sambamba na makubaliano ya kimkakati

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran amesema Tehran na Moscow zinaimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi kwa mujibu wa makubaliano ya kimkakati kupitia juhudi za mara kwa mara na azma thabiti.

Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Kitaifa la Iran aliyasema hayo Jumanne na kuongeza kuwa ni muhimu kwamba Iran na Russia  zishiriki jukumu la ziada katika soko la nishati na usafirishaji wa kimataifa.

Aliyasema hayo katika mkutano na mshauri wa ngazi za juu wa rais wa Russia, Igor Levitin, mjini Tehran.

Pia alisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya pamoja ya kiuchumi ndani ya mfumo wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya marais wa nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa Shamkhani, vikwazo vya upande mmoja vinavyoongozwa na Marekani vinazuia kupanuka kwa uhusiano baina ya nchi mbali mbali na huzidisha migogoro ya kikanda na kimataifa.

Ametoa wito wa kuundwa kwa vyombo vya pamoja ili kukabiliana na hatua za vikwazo. Amesema nchi zinazolengwa na vikwazo zinapaswa kutumia uwezo wa kimataifa kukabiliana na vikwazo hivyo.

Levitin, kwa upande wake, amesema Iran ina uwezo mkubwa katika sekta ya nishati na usafiri, na makampuni ya Russia yana nia ya kuwekeza katika miradi ya miundombinu ya Iran.

Afisa huyo wa Russia pia alirejelea makubaliano ya nchi hizo mbili ya kuendeleza uhusiano wa kibiashara kwa kutumia sarafu za kitaifa, akisema maafisa wa uchumi na benki wa nchi hizo mbili wamepitisha mbinu muhimu za kukwepa vikwazo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *