Ripoti: Marekani inasafirisha makombora hadi Ukraine kutoka kwenye maghala ya Israel

Ripoti mpya inasema Marekani inatuma kimya kimya mamia kwa maelfu ya makombora ya mizinga nchini Ukraine kutoka kwenye maghala inayodai ni yake ya dharura yaliyo katika utawala wa Kizayuni wa Israel huku vita vikiendleea kati ya Russia na taifa hilo la zamani la Shirikisho la Sovieti.

Gazeti la New York Times, likinukuu maafisa wa Marekani na utawala haramu wa Israel, limeripoti leo Jumatano kwamba Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, inatumia zana na silaha zilizo kwenye ghala kubwa la jeshi la Marekani ambazo zilikuwa zitumike katika migogoro ya Mashariki ya Kati au Asia Magharibi, ili kukidhi mahitaji ya Ukraine ya makombora na mizinga katika vita na Russia.

Washington na Tel Aviv zimekubali kusafirisha takriban makombora 300,000 hadi Ukraine, ripoti hiyo imesema, ikiongeza kuwa nusu ya silaha zinazotumwa Ukraine tayari zimesafirishwa hadi Ulaya na kufikishwa Ukraine kupitia Poland.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, maafisa wa Marekani wamekuwa wakifanya kazi nyuma ya pazia kukusanya makombora ya kutosha ili kuifanya Ukraine ijizatiti vya kutosha na silaha mwaka 2023.

Marekani imeikabidhi au kuiahidi Ukraine zaidi ya makombora milioni 1 ya milimita 155, afisa mmoja wa Marekani ameliambia gazeti la The Times, huku akisisitiza kuwa makombora hayo yamekuwa muhimu katika vita vya Ukraine.

Maafisa wa Marekani walielezea kwa mara ya kwanza uwezekano wa kuipatia Ukraine silaha kutoka kwenye akiba ya Israel mwaka jana, na hivyo kuzua wasiwasi Tel Aviv kuhusu jinsi Russia ingelitazama suala hilo. Benny Gantz, waziri wa vita wa Israel wakati huo, alijadili ombi hilo na baraza la mawaziri. Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel Yair Lapid aliidhinisha hatua hiyo baada ya mazungumzo na baraza la mawaziri na maafisa wa usalama, ripoti hiyo ilisema.

Aprili mwaka jana, Russia ilitishia Israeli kwa hatua za kulipiza kisasi ikiwa Tel Aviv ingeipatia Ukraine vifaa vya kijeshi na misaada.

Mrundiko wa silaha za kijeshi za Marekani katika utawala haramu wa Israel ulianza mwaka 1973 wakati wa Vita vya Waarabu na Waisraeli.

Russia  ilianzisha kile inachokiita “operesheni maalum ya kijeshi” dhidi ya Ukraine mwishoni mwa Februari mwaka jana kutokana na tishio la nchi hiyo kujiunga na  muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani.

Tangu wakati huo, Marekani na washirika wengine wa Ukraine wameipa nchi hiyo silaha za thamani ya makumi ya mabilioni ya dola, ikiwa ni pamoja na mifumo ya roketi, ndege zisizo na rubani, magari ya kivita, vifaru na mifumo ya mawasiliano. Nchi za Magharibi pia zimeiwekea Moscow vikwazo kadhaa vya kiuchumi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *