Chama kikuu cha upinzani cha Leba cha Uingereza kimekashifu mpango mpya wa serikali wa kutunga sheria inayolenga kuzuia migomo, kikisema kuwa hatua hiyo yenye utata inafutilia mbali uhuru wa raia.
Naibu kiongozi wa chama cha Leba Angela Rayner amesema wabunge wengi kutoka chama tawala cha Wahafidhina wa Conservative, wamewasilisha mswada huo na kwa njia hiyo, “wanavuruga uhuru ambao tuliupigania kwa karne nyingi.”
Sheria iliyopendekezwa pia imevikasirisha vyama vya wafanyakazi ambavyo vinasema kuwa itakuwa na “athari ya kukandamiza” utayari wa wafanyikazi kutekeleza haki yao ya kugoma.
Pia siku ya Jumatatu, maelfu ya waandamanaji walikusanyika nje ya lango la Downing Street huko London, iliko ofisi ya Waziri Mkuu kupinga sheria hiyo, wakiwa na mabango yaliyokuwa na maneno kama “haki ya kugoma ni haki ya kuwa na matumaini” na “mgomo wa ushindi.”
Waandamanaji wanasema uwezo wa kugoma unaruhusu wafanyakazi kubainisha haki zao na kujadiliana ili kutendewa haki na kulipwa fidia mahali pa kazi.
Serikali imewaslisha sheria mpya bungeni ambayo itawapa polisi mamlaka zaidi ya kukandamiza wanaogoma. Siku ya Jumatatu, wabunge walipiga kura kuunga mkono sheria hiyo kwa kura 309 dhidi ya 249.
Uingereza imekuwa ikikabiliana na wimbi kubwa la mgomo kwa miongo kadhaa, huku washughulikiaji wa mizigo ya viwanja vya ndege, wafanyikazi wa mpakani, wakufunzi wa udereva, madereva wa mabasi na wafanyikazi wa posta wakiacha kazi zao kudai nyongeza ya mishahara, ili kuweza kukabiliana na mfumuko wa bei unaoongezeka na kuzidi kuwa mbaya na mgogoro unaoongozeka wa gharama ya maisha. Si tu kuwa kuna ughali wa maisha nchini Uingereza bali hata kuna ukosefu wa bidhaa muhimu kama vile mayai ambayo sasa yanauzwa kwa mgao.