Bunge la Lebanon lakwama kwa mara ya 11 kumchagua Rais mpya

Bunge la Lebanon jana lilikwama tena kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo na kupelekea mkwamo wa kumchagua kiongozi wa juu zaidi nchini humo kuendelea kushuhudiwa.

Hadi sasa, vimeshaitishwa vikao kumi vya bunge la Lebanon kwa shabaha ya kumchagua rais mpya wa nchi hiyo lakini hadi sasa hakuna natija iliyopatikana.

Katika kikao kingine kilichofanya jana Alkhamisi, wabunge wa Lebanon walishindwa kwa mara ya 11 kumchagua rais mpya wa nchi hiyo.

Katika mkutano wa jana wa bunge la Lebanon, hakuna mgombea hata mmoja aliyefanikiwa kupata thuluthi mbili ya kura za wabunge wa bunge hilo ili atangazwe kuwa Rais mpya wa nchi hiyo.

Muhula wa urais wa rais wa sasa wa Lebanon Michel Aoun, ulimalizika tangu tarehe 31 Oktoba mwaka jana; na kushindwa kumchagua rais mpya kunashadidisha mgogoro wa ombwe la kisiasa la nchi hiyo kubaki bila ya rais.

Bunge la Lebanon linapaswa kumchagua Rais mpya mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa Rais aliyeko madarakani. Bunge la Lebanon lina Wabunge 128 na ili mgombea wa kiti cha urais atangazwe mshindi anapaswa kupata thuluthi mbili ya kura. Aidha kwa mujibu wa katiba, Rais wa nchi anapaswa kuchaguliwa kutoka miongoni mwa Wakristo wa Kimaroni.

Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kutumbukia Lebanon katika mkwamo wa kushindwa kumchagua Rais mpya kunaifanya anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuzidi kuwa tete sambamba na kuongeza matatizo ya kiuchumi ambayo tayari yanaiandama nchi hiyo hivi sasa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *