WHO: Vituo 97 vya huduma za afya na tiba vimesita kufanya kazi nchini Afghanistan

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema katika ripoti yake mpya kuwa vituo 97 vya afya na tiba vimesitisha sehemu ya shughuli zao au vimeacha kikamilifu kutoa huduma nchini Afghanistan.

Kwa sasa Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu, kiafya, kiuchumi na ya uhaba mkubwa wa chakula uliosababishwa na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka ishirini na jeshi vamizi la Marekani na washirika wake. Baada ya miongo miwili ya kuikalia kwa mabavu Afghanistan, na kuiteketeza miundombinu ya kiuchumi na kiafya ya nchi hiyo, mnamo Agosti 2021, Marekani iliondoa majeshi yake sambamba na vikosi vya kundi la Taliban kuingia katika mji mkuu wa nchi hiyo Kabul.
Kufuatia matukio hayo, baada ya kundi la Taliban kuingia madarakani nchini Afghanistan, Washington ilichukua hatua ya kuzuia na kuhodhi takriban dola bilioni kumi mali za wananchi wa Afghanistan na kuiwekea vikwazo nchi hiyo jambo ambalo limeifanya hali ya raia iwe mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Shafqna Afghanistan, Shirika la Afya Duniani limetangaza katika ripoti yake mpya kuhusu uwezo wa raia wa Afghanistan kupata huduma katika vituo vya afya na tiba ya kwamba vituo 79 vinavyohamishika na vituo 18 vya kudumu vimefungwa kutokana na serikali ya Taliban kuwazuia wanawake kufanya kazi.
Kulingana na ripoti hiyo, kusimamishwa kwa shughuli za vituo hivyo kumewanyima watu wapatao 500,000 fursa ya kupata huduma za dharura na muhimu za afya na matibabu.
Mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yanatahadharisha mara kwa mara kuhusu kuzorota kwa hali ya afya na kibinadamu nchini Afghanistan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *