Balozi wa Russia nchini Marekani ameonya vikali dhidi ya mashambulizi tarajiwa ya Ukraine katika Peninsula ya Crimea na kusisitiza kuwa, Moscow itajibu mapigo baada ya Washington kudokeza kuwa huenda Kiev ikatumia silaha za Magharibi kulishambulia eneo hilo.
Akitoa radiamali yake kwa kauli ya hivi karibuni ya Ned Price, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani aliyedai kuwa Crimea ni eneo la Ukraine, Anatoly Antonov, Balozi wa Russia mjini Washington amesema matamshi ya kigaidi ya US hayatakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha hali ya mambo.
Amesema Moscow katu haitoruhusu kufanyika mashambulizi katika ardhi yake ya Crimea, na kwamba hatua ya Marekani ya kudai kuwa Crimea ni milki ya Ukraine ni kuishinikiza nchi hiyo ya Ulaya Mashariki kufanya vitendo vya kigaidi dhidi ya Russia.
Jana Jumatano, Ned Price, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema vikosi vya Ukraine vipo huru kutumia silaha za Marekani eti ili kulinda mamlaka na ardhi yake ikiwemo Crimea.
Haya yanajiri siku chache baada ya gazeti la New York Times kuripoti kuwa, Marekani inatuma kimya kimya mamia kwa maelfu ya makombora ya mizinga nchini Ukraine kutoka kwenye maghala inayodai ni yake ya dharura yaliyo katika utawala wa Kizayuni wa Israel, huku vita vikiendelea kati ya Russia na taifa hilo la zamani la Shirikisho la Sovieti.
Wakati huo huo, Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ameonya kuwa, huenda vita vya nyuklia vikaibuka iwapo Russia itashindwa katika vita vya Ukraine.
Rais huyo wa zamani wa Russia amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Telegram na kueleza kuwa, “kushindwa dola (lenya silaha za) nyuklia katika vita vya ‘kawaida’ kunaweza kukachochea vita vya nyuklia.” Hata hivyo Rais Vladimir Putin alisema jana Jumatano kuwa, hakuna shaka kuwa Russia itaibuka mshindi katika operesheni zake nchini Ukraine.