Kampuni ya T-Mobile ya Ujerumani imetangaza kuwa, taarifa binafsi za makumi ya mamilioni ya wateja wa kampuni hiyo ziliibwa mwishoni mwa Novemba 2022.
Shirika la Habari la Kimataifa la Tasnim limenukuu duru za habari zikiripoti kwamba, wadukuzi wamepata data za wateja wapatao milioni 37 wa T-Mobile, ambayo ni moja ya makampuni makubwa ya simu za mkononi nchini Marekani. Kampuni hiyo ilitangaza habari hiyo baada ya kufungwa soko la hisa.
Kwa mujibu wa tangazo la kampuni hiyo, wadukuzi waliiba taarifa za watumiaji wa simu za kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na anwani, nambari za simu na tarehe za kuzaliwa za mamilioni ya watumiaji wa T-Mobile wakati walipoingia kwenye mtandao wa mawasiliano wa kampuni hiyo mwishoni mwa Novemba mwaka jana. Wataalamu wa kampuni hiyo waligundua shambulio hilo la wadukuzi tarehe 5 mwezi huu wa Januari 2023.
Sehemu nyingine ya taarifa ya kampuni ya T-Mobile imesema: Uchunguzi kuhusu uvamizi huu wa wadukuzi unaendelea, lakini inaonekana kwamba programu hasidi iliyotumika kwenye udukuzi huo sasa imezuiwa. Kampuni hiyo ya simu za mkononi nchini Marekani ilitangaza katika muendelezo wa taarifa yake kwamba imewapa taarifa maafisa wa sheria na taasisi husika kuhusu shambulio hili.
Vile vile kampuni hiyo T-Mobile imedai kuwa, shambulio hilo la wadukuzi halikuathiri huduma za mawasiliano za kampuni hiyo.