Kambi ya jeshi ya Marekani yashambuliwa kwa droni nchini Syria

Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imekiri kuwa, moja ya kambi za kistratejia za nchi hiyo huko kusini mwa Syria imeshambuliwa kwa ndege zisizo na rubani (droni).

Taarifa ya jana Ijumaa ya CENTCOM imesema kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani imeshambuliwa kwa droni katika eneo la al-Tanf, kusini mwa Syria, karibu na mipaka ya Iraq na Jordan.

Msemaji wa CENTCOM, Joe Buccino amehamakishwa na pigo hilo dhidi ya kituo cha kijeshi cha vikosi vamizi vya Marekani nchini Syria na kusema, “mashambulizi ya aina hii hayakubaliki.”

Burccino amedai kuwa, eti droni mbili kati ya tatu zilizofanya mashambulizi hayo zimetunguliwa. Hata hivyo hajaeleza ni nani amehusika na hujuma hiyo na hasara za roho na zana za kijeshi zilizosababishwa na mashambulizi hayo.

Msemaji huyo wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani amebwabwaja zaidi kwa kusema, mashambulizi ya namna hiyo yanaviweka vikosi vya nchi hiyo pamoja na vya waitifaki wake katika hatari, na eti yanakwamisha juhudi za kupambana na ISIS.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Damascus imetoa taarifa mara kadhaa ya kulaani vitendo vya vikosi vamizi vya jeshi la Marekani, sambamba na kutaka kukomeshwa uwepo haramu wa kijeshi wa Washington katika ardhi ya Syria.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kushindwa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) likiwa kama tawi la kijeshi la Marekani nchini Syria mnamo Desemba 2016, majeshi ya Marekani yalishika moja kwa moja nafasi ya kundi hilo, na kuanza wakati huohuo kuchimba na kuiba mafuta ya Syria.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *