Mashambulio ya Saudia mpakani mwa Yemen yameua watu saba na kujeruhi 91

Duru za Yemen zimeripotiwa kuwa, tangu ulipoanza mwaka mpya wa 2023 hadi sasa, watu saba wameuawa na wengine 91 wamejeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na utawala wa Saudi Arabia katika maeneo ya mpakani mwa Yemen.

Kwa uungaji mkono wa Marekani, Muungano wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia iliivamia kijeshi Yemen mwezi Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya nchi kavu, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake nchini Yemen, hadi sasa umeshateketeza roho za watu zaidi ya elfu kumi na tisa, kujeruhi makumi ya maelfu na kuwafanya mamilioni ya Wayemeni pia kuwa wakimbizi.
Televisheni ya Al-Masira imezinukuu duru za Yemen zikitangaza kuwa, tangu ulipoanza mwezi huu wa Januari hadi sasa, watu saba wameuawa na wengine 91 wamejeruhiwa katika maeneo mengi ya mpaka wa mkoa wa Saada baada ya kushambuliwa kwa risasi na makombora na jeshi la Saudia.

Wayemeni hao wameuawa wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan alidai siku nne zilizopita katika hotuba yake katika mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa Kuu la Uchumi la 2023 huko Davos, Uswisi: “vita vya Yemen inapasa viishe kwa njia ya mazungumzo na sisi tunajitahidi kutafuta njia ya kuzungumza na pande zote ili kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano”.

Kufuatia mashauriano yaliyofanywa na Umoja wa Mataifa na nia njema iliyoonyeshwa na Serikali ya Kitaifa ya Wokovu ya Yemen, usitishaji vita wa miezi miwili ulianzishwa nchini Yemen mnamo Aprili Pili, 2022, ambao ulimalizika baada ya kuongezwa kwa vipindi vingine viwili vya miezi miwilimiwili hadi Oktoba 10, 2022 bila kufikiwa makubaliano mengine mapya. Usitishaji huo wa mapigano umekiukwa mara mia kadhaa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia.
Kabla ya hapo, Serikali ya Kitaifa ya Wokovu ya Yemen ilitangaza kuwa itakubali tena kurefushwa usitishaji vita kwa sharti la kuondolewa mzingiro, kufunguliwa tena kikamilifu uwanja wa ndege wa Sana’a na kulipwa mishahara ya wafanyikazi kupitia mapato ya mafuta yanayopatikana katika mikoa inayokaliwa na mamluki wa Saudia na Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *