Mtazamo mwingine kuhusu uwekezaji mkubwa wa Bin Salman katika michezo Saudia

Iwapo mtu yeyote atafuatilia habari za Saudi Arabia baada ya kunyakuliwa madaraka ya nchi hiyo ya kifalme na Mohammed bin Salman, atakumbana na mkanganyiko mkubwa katika mielekeo na sera za nchi hiyo.

Moja ya matukio na mifano ya wazi katika uwanja huo ni kwamba, kwa upande mmoja, Bin Salman anataka kuonyesha sura inayoitwa ya kisasa ya Saudi Arabia kwa kutekeleza miradi kabambe kama ule mradi maarufu wa jiji jipya linalojulikana kama NEOM na kubadilisha mtazamo wa umma kuhusu ufalme huo wa kikabila na hivyo kujaribu kuwasilisha taswira ya utamaduni mpya. Lakini katika upande wa pili ufalme wa Saudia unatekeleza sera za mbinyo na ukandamizaji mkali wa kisiasa ambao unaambatana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Michezo pia ni mojawapo ya mbinu ambazo Bin Salman amezitumia kupotosha fikra za umma kuhusu uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo. Hivyo kuficha maovu na ukatili ni moja ya sababu ambazo zimepelekea kufanyika uwekezaji mkubwa wa Saudi Arabia katika sekta ya michezo katika zama za Bin Salman.

Kwa mujibu wa gazeti la Middle East Monitor, baada ya kufanyika mashindano ya “LIV Golf” mwaka 2022 na kandarasi ya nyota wa Ureno “Cristiano Ronaldo” na Klabu ya Al-Nasr ya mjini Riyadh, inasemekana Saudi Arabia imechukua hatua ya kununua kampuni ya Kimarekani “World Wrestling Entertainment”.

Pia, ripoti zinaonyesha kuwa klabu ya Saudia “Al Hilal” ambayo ni klabu maarufu zaidi ya soka nchini humo, inataka kumnunua “Lionel Messi”, nyota wa Argentina, kwa kiasi kikubwa cha fedha. Utawala wa Saudi pia umeshinda haki ya kuandaa kwa miaka kadhaa mashindano ya Supercopa de España ambayo huleta pamoja klabu nne kubwa za Uhispania. Hali kadhalika Saudi Arabia imetoa pendekezo kwa Ugiriki na Misri la kuandaa kwa pamoja Kombe la Dunia la FIFA la 2030.

Mnamo 2021, Saudi Arabia pia ilinunua sehemu ya hisa za kilabu cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) “Newcastle”, na pia mwaka huo huo ikaandaa mashindano ya magari ya Grand Prix ya “Formula One” na inatarajiwa kuandaa mashindano hayo tena mwaka huu.

Bila shaka, sehemu kubwa ya uwekezaji wa Saudi Arabia katika michezo unafanywa kwa ajili ya kushindana au kukabiliana na uwekezaji sawa uliofanywa na Qatar, ambayo iliweza kuandaa kwa mafanikio makubwa Kombe la Dunia la FIFA 2022.

Kwa hivyo, ni wazi kwamba harakati za Saudi Arabia na Bin Salman binafsi katika medani za michezo zimeongezeka sana baada ya michezo ya Kombe la Dunia nchini  Qatar na ndio sababu pia kutiwa saini kwa mikataba mikubwa na wanamichezo maarufu kama Ronald na Messi kumefanyika baada ya hatua hiyo.

Lakini ifahamike kuwa iwapo Qatar imefanikiwa katika sekta ya michezo, ni kwa sababu, kwanza, haijawa na matatizo makubwa ya ukiukaji wa haki za binadamu na ilijaribu kuendeleza mageuzi ya kisiasa na kiuchumi, na pili, ilitekeleza sera ya ujirani mwema na maelewano katika masuala ya eneo zima la Asia Magharibi. Serikali ya Qatar pia haijajiweka yenyewe katika hali ya kukabiliana na harakati za wananchi za kikanda, ukiwemo mhimili wa Muqawama na  Ikwanul Muslimin.

Kwa hiyo, inaonekana kwamba Bin Salman ameiweka Saudi Arabia kwenye njia sawa na ile ambayo mfalme wa kiimla, Mohammad Reza Shah, alikuwa ameiweka Iran kabla ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Kwa mujibu wa baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisiasa, kutenganisha maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya kisiasa ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha mapinduzi ya Iran.

Kwa hivyo, kuendelea mwelekeo wa sasa wa Saudi Arabia kunasababisha kuongezeka kwa pengo kati ya maendeleo ya kisiasa na maendeleo ya kiuchumi na kupelekea utawala wa Saudi Arabia kukumbana na changamoto za ndani.

Kulingana na ripoti ya Jumuiya ya Haki za Kibinadamu ya Ulaya-Saudia, utawala wa Saudi Arabia umevunja rekodi ya kuwanyonga raia katika miaka kumi iliyopita. Takwimu zinaonyesha kuwa kutoka 2013 hadi Oktoba 2022, Saudia imewanyonga watu 1100 ambapo zaidi ya 990 kati yao walinyongwa wakati wa utawala wa Mfalme Salman Bin Abdulaziz ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa Saudi Arabia mapema 2015.

Saudi Arabia hivi karibuni pia imetoa hukumu za muda mrefu na kali kwa makumi ya wafungwa, huku wengine wakikabiliwa na kifungo cha miaka kadhaa jela na wengine wakihukumiwa kunyongwa. Aidha kuna wafungwa wengi ambao wanasubiri kutolewa hukumu za kunyongwa. Kwa hiyo, inaweza kusemwa kwamba, maadamu Bin Salman anaendelea kukiuka haki za binadamu za raia wake na pia anaendeleza sera haribifu nje ya nchi kama vile uvamizi dhidi ya Yemen, uwekezaji mkubwa katika miradi ya michezo au miradi mingine mikubwa kama NEOM hautaleta maendeleo yoyote menedelevu katika nchi hiyo bali utaongeza tu migongano na migawanyiko ya ndani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *