Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameashiria kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Sweden na kueleza kuwa, nchi hiyo ya Magharibi haiwezi kuficha chuki zake dhidi ya Uislamu kwa kutumia barakoa ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.
Muhammad Baqer Qalibaf aliyasema hayo jana Jumanne wakati wa kikao cha wazi cha Bunge la Iran, ikiwa ni radimali yake baada ya kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark, Rasmus Paludan, kuchoma moto nakala ya kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu nje ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu Sweden.
Qalibaf amebainisha kuwa, “Kwanza kabisa, tunalaani vikali kitendo hicho cha fedheha cha kuivunjia heshima Qurani Tukufu nchini Sweden. Vitendo vya aina hii vinaumiza nyoyo na hisia za Waislamu na wafuasi wa dini zinazomuambudu Mungu Mmoja kote duniani.”
Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa, wanasiasa wa Sweden hawawezi kuficha chuki zao dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa kwa kujificha nyuma ya pazia la uhuru wa maoni na kujieleza.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Misri, Kuwait, Muungano wa Falme za Kiarabu, Al-Azhar ya Misri, Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu Duniani, Qatar, Saudi Arabia, Indonesia, Jordan, Morocco, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, Hizbullah ya Lebanon na Harakati za Hamas na Jihadul-Islami za Palestina ni miongoni mwa nchi na taasisi zilizochukua msimamo dhidi ya kitendo hicho cha kuchukiza, ambapo mbali na kukilaani vikali zimetaka kisirudiwe tena na kuwaadhibu wahusika wake.
Aidha Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Antonio Guterres anaunga mkono kulaaniwa vikali hatua ya kukivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu huko Sweden.