Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Tuko tayari kutoa ujuzi na uzoefu wetu, hasa katika nyanja za elimu, kilimo, uvuvi, ujenzi wa mabwawa, usimamizi wa vyanzo vya maji na kilimo umwagiliaji, ili kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za mapinduzi ya viwanda.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Hossein Amir-Abdollahian na “Stergomena Lawrence Tax”, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Tanzania, jana Alkhamisi walibadilishana mawazo kwa njia ya simu ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitilia mkazo nia ya nchi yake ya kusaidia juhudi za Tanzania za kuwa nchi ya viwanda.
Katika mazungumzo hayo kwa njia ya simu, mawaziri hao wawili wa mambo ya nje wamejadiliana pia masuala yenye maslahi na maendeleo ya ushirikiano wa pamoja.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kumpongeza Bi Stergomena Lawrence Tax kwa kuteuliwa kuwa Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Tanzania amesisitizia ulazima wa kustawishwa ushirikiano wa pamoja katika nyuga mbalimbali na kuongeza: “Kwa bahati nzuri, nchi hizi mbili zina mitazamo inayofanana katika majukwaa ya kimataifa na siku zote kipaumbele cha nchi hizi mbili ni kustawisha mahusiano baina yao hasa katika nyanja za biashara na uchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Tuko tayari kuipa Tanzania ujuzi na uzoefu wetu katika maendeleo na uwekezaji wa kuifanya nchi hiyo kuwa ya viwanda, hasa katika nyanja za elimu, kilimo, uvuvi, ujenzi wa mabwawa, usimamizi wa vyanzo vya maji na kilimo cha umwagiliaji.