Ikiwa ni katika kuendeleza ugaidi na jinai dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, Alkhamisi asubuhi, baraza la mawaziri lenye misimamo mikali ya kupindukia mipaka la utawala wa Kizayuni lilitekeleza jinai nyingine ya kutisha dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika kambi ya wakimbizi huko Jenin.
Jana asubuhi, askari wa utawala wa Kizayuni huku wakisaidiwa moja kwa moja na maafisa wa usalama wa kikosi cha Shabak, walishambulia kambi ya Jenin, ambapo walikabiliana na wanamapambano wa Palestina waliosimama kutetea haki na usalama wa familia zao. Katika shambulio hilo, Wapalestina 10 waliuawa shahidi na wengine 16 wakajeruhiwa. Bado kuna uwezekano wa kuongezeka idadi ya mashahidi wa jinai hiyo ya umwagaji damu.
Licha ya kuwa vyanzo vya habari vya Kizayuni vimetaja sababu ya kutekelezwa hujuma hiyo na askari katili wa Israel kuwa ni katika juhudi za kukamatwa mwanachama mmoja mashuhuri wa Harakati ya Jihad Islami na vile vile kuzuia operesheni za muqawama wa Palestina, lakini jinai hiyo inahusiana moja kwa moja na misimamo ya kupindukia mipaka ya baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu linalotawala sasa katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
Baraza jipya la mawaziri la Netanyahu ndilo baraza la mawaziri lenye misimamo mikali zaidi katika historia ya miaka 75 ya utawala wa Kizayuni, na baadhi ya mawaziri wake akiwemo waziri wa usalama wa ndani ni wabaguzi wa rangi wasioficha ubaguzi wao, magaidi na wakorofi wasio na haya. Baraza hilo la mawaziri linaendesha rasmi ugaidi na ghasia dhidi ya Wapalestina na linatumia zana zake zote kwa ajili ya kuwakandamiza Wapalestina wasio na hatia. Kuhusiana na hilo, katika siku za karibuni, Itamar Ben Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa Israel, alizungumzia suala la kutumia askari na maafisa wa Intelejensia na Usalama wa Ndani (Shabak) dhidi ya Wapalestina, na askari hao katili pia walitumika katika jinai iliyotekelezwa jana asubuhi.
Unyama wa jinai za jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina ni wa kutisha kiasi kwamba hata mwandishi wa habari wa kijeshi wa kanali ya Kizayuni ya Kan alisema kwamba operesheni iliyofanywa huko Jenin haikuwa ya kawaida. Hisham Qassem, mjumbe wa uongozi wa harakati ya Hamas nje ya mipaka ya Palestina amesema: “Jinai ya umwagaji damu ambayo utawala wa Kizayuni umeianzisha leo asubuhi katika kambi ya Jenin ni dhihirisho la kivitendo la mbinu zinazotumiwa na serikali mpya ya mrengo wa kulia ya Israel ambapo maafisa na askari wa utawala huo wamepewa ruhusa ya kutumia silaha nzito dhidi ya raia wa kawaida wa Palestina.”
Suala jingine muhimu ni kwamba jinai hiyo imesadifiana na zoezi la pamoja la kijeshi kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni, safari ya Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na safari ya Benjamin Netanyahu huko Jordan. Matukio hayo ya kisiasa ni njia salama kwa baraza la mawaziri la Netanyahu lenye itikadi kali kwa ajili ya kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina. Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni linaamini kuwa halitakabiliwa na radiamali yoyote ya kigeni katika kudumisha jinai hizo dhidi ya taifa la Palestina, na kwamba hata nchi za Kiarabu zitatosheka tu kwa kutoa taarifa zisizokuwa na uzito wowote katika kulaani ukatili huo unaotekelezwa na Wazayuni dhidi ya ndugu zao.
Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa jinai hizo ni matokeo ya moja kwa moja ya uamuzi wa nchi vibaraka za Kiarabu wa kuanizsha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ambao umepelekea kuwekwa pembeni suala la Palestina katika ulimwengu wa Kiarabu, na pia zimechangiwa na kimya cha taasisi muhimu za kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambazo zimekataa kuchukua hatua yoyote ya maana katika uwanja huo.
Kuhusiana na hilo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar imetoa taarifa ikilaani jinai iliyotekelezwa karibuni na Wazayuni huko Jenin na kusema: “Israel inayokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina hivi sasa imepata imani kuliko wakati mwingine wowote kwamba haitawajibishwa wala kuadhibiwa kimataifa kutokana na jinai zake hizo. Suala hilo ndilo limeishajiisha iendelee kufanya jinai na uchokozi zaidi dhidi ya ndugu zetu wa Kipalestina na kuua raia bila kujali lolote.”
Hata kama jamii ya kimataifa haijachukua na wala haitachukua hatua yoyote dhidi ya jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina, lakini jinai hizo na hasa iliyotekelezwa jana huko Jenin, zitakabiliwa na jibu kali kutoka kwa Wapalestina. Bila shaka jinai hizo zitaimarisha moyo wa mapambano na umoja miongoni mwa Wapalestina, kuongeza mapigano kati ya Wapalestina na Wazayuni na ni wazi kuwa ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni hazitakuwa salama kutokana na operesheni za mapambano za Wapalestina. Hayo, kwa hakika, ni matokeo muhimu ya kuingia madarakani baraza la mawaziri lenye itikadi kali la Netanyahu katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu, jambo ambalo baadhi ya shakhsia na maafisa wa Israel walikuwa wameonya juu yake huko nyuma.