Waziri Mkuu wa Italia, Bi Giorgia Meloni Jumatatu wiki hii alifanya ziara ya siku mbili nchini Algeria na kutia saini mikataba kadhaa ya kuongeza kiwango cha kuingia barani Ulaya gesi nyingi zaidi ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanywa kwa pamoja baina ya Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria siku ya Jumatatu, Rais wa Algeria alisema kuwa, pande mbili zimetiliana saini mikataba kadhaa ukiwemo wa kujenga bomba jipya la gesi, mradi ambao alisema, utaifanya Italia kuwa msambazaji mkuu wa nishati ya Algeria barani Ulaya.
Kwa upande wake, Meloni alisema kuwa, kutokana na mgogoro na msukosuko wa nishati barani Ulaya, Algeria inaweza kuwa moja ya wasambazaji waanzilishi wa nishati inayohitajika barani Ulaya katika ngazi za bara la Afrika na kimataifa, akibainisha kwamba, Algeria ni mshirika nambari moja wa kibiashara wa Italia barani Afrika. Pia alielezea matumaini yake ya kubadilishana uzoefu na kuimarishwa ushirikiano baina ya Rome na Algiers, hasa katika maeneo ya miundombinu ya dijitali, mawasiliano, biomedicine, viwanda na nishati mbadala. Algeria na Italia zimetiliana saini mikataba kadhaa mingine ya ushirikiano wakati wa sherehe za kutiwa saini mkataba huo wa bomba jipya la gesi, sherehe ambazo ziliongozwa na Rais Tebboune na Waziri Mkuu Meloni.
Ukweli ni kuwa, nchi za Ulaya hivi sasa zina mgogoro mkubwa wa nishati uliopelekea kupaa bei za bidhaa na mfumuko wa bei baada ya nchi hizo kuiwekea vikwazo vikubwa Russia ambayo ndiye mdhamini mkuu wa gesi barani Ulaya. Nchi hizo za Ulaya zimejifanya kusamehe gesi na nishati ya bei nafuu ya Russia kwa kisingizio cha vita vya Ukraine na kile walichodai kulinda heshima yao, lakini hadi hivi sasa zinaendelea kutumia nishati ya nchi hiyo na zimeshindwa kupata nishati mbadala. Miji mbalimbali ya Ulaya hivi sasa inashuhudia maandamano makubwa ya wananchi ya kulalamikia ughali wa maisha. Maandamano makubwa ya karibuni ni yale yaliyofanyika katika mji wa Lausanne nchini Uswisi kulalamikia kiwango cha chini cha mishahara, ugumu wa maisha na kupanda bei za bidhaa ambako hakuendani na mishahara ya wafanyakazi. Wiki chache zilizopita pia kulifanyika maandamano mengine kama hayo nchini Uswisi ambapo waandamanaji walitishia kuwa, kama viongozi wa nchi hiyo ya Ulaya hawatosikiliza madai ya wananchi, basi maandamano mengine yatafanywa nchini humo tarehe 31 mwezi huu wa Januari, 2023.
Kwa upande wake, shirika la habari la Bloomberg limetangaza kuwa, baada ya Russia na Norway, Algeria ni nchi ya tatu kwa kusafirisha gesi kwa wingi duniani na ni nambari moja kwa kuzalisha kwa wingi gesi barani Afrika. Ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi za Ulaya zinaiangalia kwa tamaa kubwa gesi ya nchi hiyo. Lakini pamoja na hayo, akiba ya gesi ya Algeria si ya kiwango cha kuweza kuziba pengo la gesi ya Russia, barani Ulaya.
Mbali na ripoti hiyo ya Bloomberg, wataalamu wengine wanasema kuwa, sababu ya viongozi wa nchi za Ulaya kupigana vikumbo huko Algeria ni kila mmoja kutaka kufaidika zaidi na nishati ya nchi hiyo kuliko wenzake. Italia hivi sasa ndiye msafirishaji mkuu wa gesi ya Algeria kuelekea barani Ulaya kutokana na miundombinu yake ya kusafirisha gesi kibisahara. Bomba la gesi la Trans-Mediterranean lilijengwa mwaka 1983 ambalo linasafirishaji gesi ya Algeria hadi kwenye fukwe za Italia. Kila siku bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha zaidi ya mitakubiki milioni 110 za gesi, ingawa hivi sasa linasafirisha chini ya asilimia 60 ya uwezo wake.
Katika ziara ya Waziri Mkuu wa Italia huko Algeria, pande mbili zimetiliana saini makukbaliano ambayo yataiwezesha Itali kuongeza kiwango chake cha kununua gesi ya Algeria, kutoka mitakubiki bilioni 20 hadi mitakubiki bilioni 35 za gesi kwa mwaka. Vile vile Italia ina nia ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 iweze kuingiza nchini humo mitakubiki bilioni 50 hadi bilioni 70 za gesi ya Algeria kwa mwaka, ili iwe kitovu cha kusambaza gesi barani Ulaya. Tab’an yote hayo yatategemea uwekezaji mkubwa na hali ya kisiasa na kiuchumi ya Algeria, huko kaskazini mwa Afrika.