Guterres akosoa nafasi ya mtandao wa intaneti katika kueneza chuki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba sehemu kubwa ya mtandao wa intaneti imekuwa dampo la taka za sumu zinazoeneza chuki na uongo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema katika taarifa yake kwamba mtandao wa intaneti una aina mbalimbali za chuki, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya wageni, chuki dhidi ya Wayahudi na chuki dhidi ya wanawake.

Kwa mujibu wa Guterres, sehemu nyingi za mtandao wa intaneti sasa zimekuwa dampo la taka za sumu za kuibua chuki na uwongo wenye shari, na kuna ulazima wa kuanzishwa mchakato wa ulinzi wa haraka dhidi ya matamshi ya kuchukiza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameonya kwamba ulimwengu unakabiliwa na itikadi kali na ugaidi, na kwamba tishio hili linaongezeka; na kasi ya kuongezeka kwa tatizo hili inashuhudiwa katika ulimwengu wa mtandao wa intaneti.

Guterres amesema, kwa kutumia algorithimu zinazozidisha chuki na uhasama, watumiaji wa mitandao ya intaneti na vyombo vya habari huvutiwa na tovuti za aina mbalimbali, na majukwaa ya mitandao ya kijamii yanahusika katika suala hilo huku waenezaji wa propaganda wakizidisha biashara zao kwa kutumia mtindo huu.

Ikumbukwe kuwa, mwezi Disemba mwaka jana taasisi ya Pew ilichapisha matokeo ya uchunguzi uliofanyika kwenye nchi 19 duniani, ambapo asilimia 84 ya wahojiwa katika nchi hizo walisema kuwa, mitandao ya kijamii na intaneti ni vituo vinavyotumiwa kirahisi kueneza chuki na uvumi na kuathiri akili ya umma kwa kutoa taarifa za uongo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *