Jumapili ya juzi tarehe 5 Februari wananchi wa Sudan waliandamana katika mji mkuu Khartoum kwa shabaha ya kupinga hatua ya utawala wa kijeshi nchini humo ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waandamanaji hao sambamba na kulaani safari ya siku ya Alhamisi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala haramu wa Israel Eli Cohen aliyetembelea Sudan ambapo alikutana na mkuu wa jeshi na kiongozi wa nchi hiyo, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan walisikika wakipiga nara dhidi ya Israel.
Waandamanaji waliokusanyika katikati mwa Khartoum pia walipeperusha mabango ya kulaani kuhalalisha uhusiano kati ya Sudan na utawala ghasibu wa Israel.
Miongoni mwa mabango yaliyopeperushwa na waandamanaji yalikuwa yana maandishi kama vile “Palestina haiuzwi” na “Khartoum haitasaliti Al Quds”.
Kadhalika waandamanaji hao waliokuwa na hasira walitangaza wazi kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ni khiyana na usaliti. Maandamano hayo yalifanyika kwa mwaliko na uratibu wa Muungano wa Wasudan Dhidi ya Kuanzisha Uhusiano wa Kawaida na Israel ambao ulianza rasmi harakati zake Februari 2020.
Muhammad al-Mubarak, mweledi na mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Kisudan anasema: Msimamo wa wananchi wa Palestina kuhusiana na kadhia ya Palestina uko imara na thabiti na daima wataendelea kuwa pamoja na taifa la Palestina na hawakubaliani katu na suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel.
Ijumaa ya tarehe 23 Oktoba, 2020 Rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa Sudan na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida ikiwa na maana ya Sudan kujiunga na nchi zingine za Kiarabu na Kiislamu za Misri, Jordan, Imarati na Bahrain kuutambua rasmi utawala huo haramu unaoikalia kwa mabavu Palestina na Quds tukufu.
Nchi kadhaa za Kiarabu zimeamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ilhali kwa miaka na miaka sasa utawala huo wa Kizayuni umekuwa ukiendeleza jinai na ukandamizaji dhidi ya wananchi madhulumu wa na kuyakalia kwa mabavu maeneo mengi ya ardhi za nchi za Kiislamu na Kiarabu.
Kuanzia mwaka 1958 hadi tarehe 20 Aprili 2021, Sudan ilikuwa na sheria ambayo ilikuwa ikipiga marufuku kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel. Aidha sheria hiyo ilikuwa ikitambua kufanya biashara na Wazayuni, kuwa na uhusiano wa kibiashaara na mashirika ya Israel au yenye maslahi na Israel ni kinyume cha Sheria kama ambavyo ilikuwa ikipiga marufuku kuingiza nchini Sudan moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja bidhaa za Israel.
Licha ya hayo yote, lakini hatimaye Sudan nayo iliamua kufuata mkumbo wa baadhi ya madola ya Kiarabu kupitia mpango mchafu uliopigiwa upatu na aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo Donald Rump wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Lengo la Sudan la kufikia uamuzi huo lilikuwa ni kuiridhisha Marekani na hivyo kuifanya iliondoe jina la nchi hiyo katika orodha yake ya eti mataifa yanayounga mkono ugaidi. Katika hatua ya awali, Sudan ilikubali kulipa fidia ya dola milioni 335 manusura wa milipuko katika balozi za Marekani jijini Dar es Salaam Tanzania na Nairobi Kenya iliyotokea 1998. Siku tano baadaye, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan ikatangaza kuwa, imefikia makubalino na Waziri wa Mashauri ya Kigenii wa Iisrael kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo.
Licha ya kuwa nchiini Sudan kumekuwa kukifanyika maandamano mara kwa mara ya kuliunga mkono taifa la Palestina na kulaani nchi yao kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel, lakini maandamano ya juzi yalichochewa na safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel mjini Khartoum. Katika safari hiyo, ambapo Eli Cohen alikutana na kufanya mazungumzo na Jeneral al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo, pande mbili zilisisitiza kuwa, zimeazimia kupanua zaidi wigo wa ushirikiano. Cohen ambaye alionekana kuridhishwa na safari yake hiyo nchini Sudan amesema, kuwa ilikuwa safari ya kihistoria.
Ukweli wa mambo nii kuwa, Sudan ambayo kwa sasa inatawaliwa na majerali wa jeshi kwa uongozi wa Jenerali Abdul-Fatah al-Burhan imefikia uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ili kuiridhisha Marekani na kupata himaya ili iendelee kubakia madarakani.
Pamoja na hayo kufanyika maandamano ya wananchi ya kupinga mpango huo ni ishara ya wazi kwamba, Baraza la Utawala la Sudan linakabiliwa na kibarua kigumu katika njia ya kufikia malengo yake hayo.