Mali yalaani matamshi ya Rais wa Baraza la Ulaya

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali imelaani vikali matamshi yaliyotolewa hivi majuzi na Rais wa Baraza la Ulaya dhidi ya serikali ya nchi hiyo akiyataja kuwa yanaingilia mambo ya ndani ya Mali.

Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Ulaya hivi karibuni alidai kuwa serikali ya Mali inasambaratika baada ya kukata muungano wake wa kijeshi na nchi za Ulaya dhidi ya makundi ya waasi nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali, imeeleza kuwa, matamshi ya Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, kuhusu kusambaratika kwa serikali ya Mali “siyo ya kirafiki”, ” ni makosa” na ya “kichokozi”.

Taarifa hiyo imesema kuwa madai ya Rais wa Baraza la Ulaya ni kielelezo cha “kampeni ya upotoshaji” dhidi ya serikali ya Mali.

Uhusiano wa nchi ya Mali na Ulaya, haswa na Ufaransa, umekuwa ukidorora kwa muda mrefu.

Uhusiano huo ulizidi kuwa mbaya baada ya wanamgambo wa Wagner kutoka Russia kuingia Mali, kiasi kwamba vikosi vya jeshi la Ufaransa vilivyokuwepo nchini Mali kwa takriban miaka 10 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, vimelazimika kuondoka nchini humo.

Baraza la Kijeshi la Mali limepiga marufuku shughuli zozote za mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafadhiliwa kifedha na Ufaransa.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali, Abdoulaye Diop, alimwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kumueleza kwamba: Ufaransa imekiuka mara kadhaa anga ya nchi hiyo na imewapatia silaha nyingi magaidi wenye misimamo ya kufurutu mpaka.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *