Wapinzani nchini Kenya wamefanya tena maandamano leo dhidi ya serikali kwa ajili ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Maanadamano hayo yamefanyika tena leo baada ya upinzani kuapa kuwa maandamano hayo yatafanyika licha ya marufuku ya Jeshi la Polisi.
Vikosi vyya usalama jijini Nairobi vimekabiliana na waandamanaji hao na kuwatawanya vikitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi.
Kinara mkongwe wa upinzani Raila Odinga ameapa kuwa maandamano hayo yataendelea licha ya marufuku ya polisi na amewataka wananchi kujitokeza barabarani kila siku ya Jumatatu na Alkhamisi, licha ya maandamano ya wiki iliyopita kuzusha ghasia na vurugu.
Kabla ya maandamano hayo, usalama uliimarishwa huku polisi wa kutuliza ghasia wakiwa katika maeneo ya kimkakati jijini Nairobi na kufanya doria mitaani, huku maduka mengi yakiwa yamefungwa na huduma za treni kutoka viunga vya mji mkuu hadi katikati ya jiji zikisitishwa.
Wizara ya mambo ya ndani ya Kenya inapendekeza mabadiliko ya sheria za usalama ambayo yatafanya iwe vigumu kwa watu kufanya maandamano.
Wiki iliyopita, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Maseno alipigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na Azimio la Umoja One Kenya.
Ruto amemtuhumu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwa anajaribu kuanzisha mgogoro kwa mara ya pili, nchini Kenya kama ule wa baada ya uchaguzi wa 2017 uliomlazimisha Rais wa wakati huo, Uhuru Kenyatta, kufikia makubaliano ambayo yalimpa mapendeleo ya serikali.