Mjumbe wa Baraza Kuu la Yemen: Tumejiweka tayari kwa chaguo lolote lile itakaloamua Saudia

Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema, “tumejiweka tayari kwa machaguo yote; ikiwa muungano wa Saudia utataka suluhu, sisi ni watu wa suluhu na ikiwa wanataka vita pia, sisi tumepata uzoefu wake kwa miaka minane”.

Siku mbili zilizopita, jumbe za Saudi Arabia na Oman ziliwasili mji mkuu wa Yemen, Sana’a kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na Mahdi Al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen. Wawakilishi wa jumbe hizo kutoka Riyadh na Muscat wanatazamiwa kujadiliana na Al-Mashat kuhusu kuondolewa mzingiro pamoja na athari zake zote, kusimamishwa uchokozi na kurejeshwa haki za watu wa Yemen, ikiwa ni pamoja na kulipwa mishahara ya wafanyakazi wa serikali kutokana na mapato ya mafuta na gesi.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Mayadeen, Muhammad Ali al-Houthi, Mjumbe wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen alisisitiza siku ya Jumatatu kuwa, mazungumzo na Saudi Arabia, ikiwa ndiyo nchi inayoongoza muungano wa Waarabu baada ya Marekani, yatafanyika kwa msingi huo na matokeo yake yatatangazwa rasmi kwa wananchi wa Yemen.

Al-Houthi amekosoa muelekeo wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia na kueleza kwamba katika kila duru ya mazungumzo, adui hujaribu kueneza uvumi na kuvujisha habari kuhusu mazungumzo hayo.
Kuhusiana na hilo, Balozi wa Saudi Arabia Mohammad bin Saeed Al Jaber alisema Jumatatu hiyo hiyo kwamba ziara yake huko Sana’a imefanyika kwa lengo la kuendeleza usitishaji vita sambamba na kuchunguza na kutafuta njia za kuendesha mazungumzo kati ya Wayemen wenyewe na kufikia suluhu kwa njia za kisiasa.
Al-Jaber aliongeza kuwa, yeye pamoja na ujumbe wa serikali ya Oman, wamekwenda Sana’a kwa lengo la kuendeleza usitishaji vita, kusimamisha mapigano na kuunga mkono zoezi la ubadilishanaji mateka wa vita…/
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *