Farhan Haq, naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hali nchini Sudan inapaswa kudhibitiwa haraka iwezekanavyo, na kwamba Umoja wa Mataifa unafanya jitihada za kupatikana usitishaji vita wa muda mrefu zaidi nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, matamshi hayo ya naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa yamekuja huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa mara nyingine tena akizitaka pande zinazohusika katika mzozo wa Sudan kusitisha mara moja mzozo huo na kutangaza kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kushirikiana kwa karibu na washirika wake ili kupunguza mvutano na kuanzishwa usitishaji vita wa kudumu nchini Sudan.
Migogoro ya kijeshi nchini Sudan ulianza asubuhi ya Jumamosi, Aprili 15, 2023 kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Radiamali ya Haraka. Mzozo huo wa kuwania madaraka umeshasababisha kupotea roho za watu wengi na uharibifu mwingine mkubwa wa mali za umma.
Ingawa kumetangazwa makubaliano ya kusimamisha vita kwa muda wa siku tatu, lakini upatanishi wa kimataifa wa kumaliza mzozo na kuzifanya pande hasimu ziache ugomvi baina yao, haujazaa matunda yanayotakiwa hadi hivi sasa.
Mapigano makali yameendelea kuripotiwa kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Radiamali ya Haraka katika maeneo mawili ya mji wa “Al-Khartoum Bahri” kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan.
Huku hayo yakiendelea, jitihada za kila nchi za kuwaondoa watu wake nchini Sudan zinaendelea na bado hali si shwari nchini humo.