Mivutano mipya inazuka katika Msikiti wa Al-Aqsa sambamba na kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Sababu ni kuwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel baada ya kukabiliwa na hatari ya kufunguka medani mpya za mapambano kutokea Gaza, kusini mwa Lebanon na Golan ya Syria kwa ajili ya kuzuia mashambulizi na uvamizi zaidi wa Wazayuni, aliwakataza Wazayuni kuingia Msikiti wa Al-Aqsa hadi mwisho wa mwezi wa Ramadhani, suala ambalo wakati huo lilikabiliwa na upinzani mkubwa wa Wazayuni, akiwemo Waziri wa Usalama wa Ndani, Itamar Ben-Gvir.
Tangu mwanzoni mwa mwezi uliomalizika wa Ramadhani, Msikiti wa Al-Aqsa ulishuhudia ongezeko la mivutano na migogoro kati ya waumini wa Kipalestina na wanajeshi wa Kizayuni kandokando ya Msikiti wa Al-Aqsa na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kilele cha mzozo huo kilikuwa mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na mapigano na Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala. Wakijibu hujuma hizo, wanaharakati wa Kambi ya Muqawama walivurumisha mamia ya maroketi kutoka kusini mwa Lebanon na Ukanda wa Gaza kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Kwa kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni baada ya wanajeshi wa Israel kuwashambulia waumini katika Msikiti wa Al-Aqsa, Wapalestina walimlazimisha Benjamin Netanyahu kufuta uamuzi wake kuhusu Msikiti wa Al-Aqsa na kuwazuia Mayahudi kuingia katika msikiti huo hadi mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Haya yanajiri licha ya kuwa kabla ya hapo ilitangazwa kuwa walowezi wa Kiyahudi wanaruhusiwa kushambulia Msikiti wa Al-Aqsa katika muda wa siku 10 za mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Kuongezeka umoja na mshikamano wa ndani na nje baina ya Wapalestina na ushiriki wa wanaharakati katika kuuhami na kuulinda Msikiti wa Al-Aqswa na kuanzishwa mapambano ya ndani na nje katika kuitetea Palestina hususan Msikiti wa Al-Aqsa, ni miongoni mwa sababu za kurudi nyuma na kulegeza kamba huko.
Kwa hiyo, ilitazamiwa kwamba baada ya kumalizika mwezi wa Ramadhani, mashambulizi na uchokozi wa Wazayuni utaanza tena, na Jumamosi, siku ya pili ya Idul Fitr, wavamizi wa Israeli walishambulia eneo la Bab al-Rahma katika Msikiti wa al Aqsa na kuvunja milango yake. Ripoti zinaonyesha kuwa uharibifu mkubwa ulifanywa katika eneo hilo takatifu katika shambulio la Wazayuni kwenye Msikiti wa al Aqsa.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Palestina (Hamas) ililaani vikali shambulio hilo la Israel kwenye eneo la Bab al-Rahma katika Msikiti wa Al-Aqsa. Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem, amesisitiza kuwa, mashambulizi ya wanajeshi wa Israel katika eneo la Bab al-Rahma na uharibifu uliofanywa eneo hilo la Msikiti wa al Aqsa vinadhihirisha azma ya Wazayuni ya kuendeleza vita vya kidini dhidi ya maeneo matakatifu ya Quds. Hii ina maana kwamba vita vya kutaka kubadilisha utambulisho wa Msikiti wa Al-Aqsa vinaendelea.
Tariq Salmi, msemaji wa harakati ya Jihad Islami, pia amesema kuwa eneo la Bab al-Rahma ni sehemu muhimu ya Msikiti wa Al-Aqswa, na amesisitiza kwamba juhudi za adui za kutaka kudhibiti msikiti huo hazitafua dafu, na mashambulizi yoyote dhidi ya Msikiti wa Aqsa na maeneo matukufu ya Quds yatakuwa na madhara makubwa kwa eneo zima la Magharibi mwa Asia.
Uamuzi mwingine ambao Wapalestina wameuchukua kukabiliana na uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kuendelea kuhudhuria na kufanya ibada kwenye Msikiti wa Al-Aqsa. Idadi ya waumini waliohudhuria Swala ndani ya Msikiti wa Al-Aqsa katika mwezi wa Ramadhani ilifikia zaidi ya watu milioni 4 licha ya vikwazo vya Israel, na sasa wanaendelea kuhudhuria ibada ndani ya msikiti wa huo baada ya mwezi wa Ramadhani.
Kuhusiana na suala hilo, Sheikh Hussein Abu Kuik, mmoja kati ya viongozi wa harakati ya Hamas amesisitiza ulazima wa kuendelea kuhudhuria Swala na ibada katika Msikiti wa Al-Aqsa baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ili sehemu hiyo tukufu ilindwe mbele ya njama na hujuma za askari wa Israel na walowezi wa Kiyahudi.
Ahmed Attoun, mwakilishi wa Bunge la Palestina kutoka mji wa Quds, pia amewatolea wito Wapalestina wa kuendelea kuhudhuria kwa wingi katika Msikiti wa Al-Aqsa baada ya mwezi mtukufu ili kushinda njama za Israel dhidi ya msikiti huo mtukufu.
Miito hii inaonyesha kuwa Wapalestina walioko ndani bado wako mstari wa mbele kuuhami Msikiti wa Al-Aqswa, lakini wakati huo huo wanatarajia kuwa Wapalestina na vikosi vya muqawama nje ya Palestina, vitaendelea kujipanga kikamilifu kuzuia shambulio lolote dhidi ya Msikiti wa al Aqsa.