Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Profesa Kithure Kindiki amesema, mauaji ya waumini wa Kanisa la kijiji cha Shakahola kilichoko katika Kaunti ya Kilifi ni hatua ya mabadiliko makubwa na muhimu kwa nchi hiyo kuhusu jinsi ya kushughulikia masuala ya usalama yanayosababishwa na waasi wa kidini.
Kindiki ameyasema hayo huku ripoti kutoka nchini Kenya zikieleza kuwa idadi ya watu waliofariki kutokana na njaa kali, wakiwa miongoni mwa wafuasi wa kanisa lenye utata la Good News International linalomilikiwa na mhubiri Paul Makenzie Nthenge, imefikia 89 baada ya miili sita mingine ukiwemo wa mtoto kufukuliwa kwenye kaburi moja msituni huko Shakahola leo mchana.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili eneo la zoezi hilo la ufukuaji wa miili ya wahanga wa kanisa hilo amebainisha kuwa, hayo yalikuwa matumizi mabaya ya haki za kimsingi za uhuru na kudai kuitumia Biblia kwa ajili kuua na kusababisha mauaji ya halaiki.
Kindiki ameongezea kwa kusema, wale waliowahimiza wengine kufunga na kufa walikuwa wakila na kunywa huku wakidai kuwatayarisha wahanga hao kukutana na muumba wao.
Amesisitiza pia kuwa, Mackenzie na washirika wake watahukumiwa tu kwa matendo yao na lazima wapewe adhabu kali kwa maisha yaliyopotea na maumivu waliyoyasababisha kwa wanadamu wenzao.
Wakati huohuo, waziri huyo wa mambo ya ndani wa Kenya amesema serikali inachunguza waumini wengine pia wa kidini katika kaunti hiyo ya Kilifi wanaotumia dini kuwalaghai Wakenya.
Leo asubuhi, polisi walipata miili 10 zaidi, ikiwa ni watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa madhehebu hiyo ya Kikristo ambao waliaminishwa kuwa wangeweza kwenda mbinguni kama wangeshinda na njaa.
Aidha, wamewaokoa wanawake wawili ambao walikuwa wamedhofu sana kwa njaa kali wakionekana kukaribia kufa. Wahanga hao walikimbizwa katika hospitali ya Malindi mkoani Pwani kwa ajili ya matibabu…/