Doha, mji mkuu wa Qatar, ambayo katika miaka ya hivi karibuni umekuwa mwenyeji wa duru kadhaa za mikutano mbalimbali kuhusu Afghanistan, kuanzia jana ulikuwa tena mwenyeji wa mkutano wa siku mbili unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ambao unahudhuriwa na wawakilishi maalumu wa nchi 25 na mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya Afghanistan.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa mwenyeji wa Mkutano wa Doha, alitangaza baada tu ya kuwasili Qatar kwamba: Mkutano huu, utajadili jinsi ya kuamiliana na serikali ya Taliban huko Afghanistan ili kufikia maelewano ya pamoja ya kimataifa.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza katika taarifa yake kuwa: Katibu Mkuu wa umoja huo atakuwa mwenyeji wa wawakilishi wa nchi za dunia kwa ajili ya Afghanistan katika siku za tarehe 11 na 12 Mei ili kufikia mwafaka kuhusu masuala muhimu ya Afghanistan kama vile haki za binadamu hususan haki za wanawake na wasichana, kuundwa serikali jumuishi, na mapambano dhidi ya ugaidi na madawa ya kulevya.
Umoja wa Mataifa hapo awali ulikataa suala la kulitambua rasmi kundi la Taliban katika mkutano wa Doha; hata hivyo sasa inaonekana kwamba ushirikiano na Taliban ndio lengo kuu la mkutano wa sasa kuhusu Afghanistan.
Wakati huo huo, Waafghani wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya dunia wamefanya maandamano wakipinga suala la kutambuliwa kundi la Taliban, na wamezitaka nchi za ulimwengu zisilitambua rasmi kundi hilo. Maandamano hayo yalianza baada ya kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed, kuhusu “kuchukuliwa hatua ndogo ya kuitambua Taliban” na kutangaza wakati wa mkutano wa Doha, chini ya uenekiti wa Antonio Guterres.
Malalamiko hayo yameonyeshwa kwa njia tofauti hadi sasa; kuanzia maandamano ya mitaani hadi kutuma barua za wazi wanawake, wadau wa masuala ya utamaduni, watetezi wa haki za binadamu, na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika mkesha wa mkutano wa Doha, kundi la mashirika ya kiraia na wafanyakazi wa kutoa misaada nchini Afghanistan lilitoa wito wa kuongezeka jumbe za kidiplomasia za nchi mbalimbali nchini Afghanistan, kuzidishwa maingiliano ya moja kwa moja na mazungumzo na Taliban, kuachiliwa fedha za Afghanistan, na kuondolewa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo.
Kama inavyoonekana, wananchi na kund linalotawala Afghanistan la Taliban wana matarajio tofauti kwa mkutano wa Doha; kwani wakati Taliban wanatarajia kutambuliwa rasmi katika mkutano huu, wapinzani, haswa wanawake, wanatarajia kwamba mkutano wa Doha utachukua hatua za dharura za kulilazimisha kundi la Taliban kudhamini haki za wanawake.
Kwa msingi huo, Hassan Kazemi Qomi, mwakilishi maalumu wa Rais wa Iran katika masuala ya Afghanistan anasema, msimamo wa Tehran katika mkutano wa Doha ni huru na wa kujitegemea, na unazingatia uhalisia wa hali ya sasa na maslahi ya watu na serikali ya Afghanistan.
Qomi ambaye pia ni balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kabul amesema: Maoni ya umma katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanasubiri kuona mambo mawili ili kuweza kutoa kuhukumu kuhusu utawala wa Taliban: Kwanza ni katiba ya serikali, na pili ni kushuhudia hatua za kweli za serikali hiyo za kutekeleza majukumu yake ya kimataifa.
Moja kati ya mikakati ya Iran ni kuunga mkono mazungumzo ya ndani ya Waafghani wenyewe. Tangu kumalizika mkutano wa Born mwaka 2001, Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikisisitiza kwamba, makabila na kaumu zote za Afghanistan zinapaswa kuwa na nafasi sawa katika utawala na mamlaka ya kisiasa ya nchi hiyo, ili amani na utulivu viweze kuimarishwa nchini Afghanistan.
Pendekezo la kuanzishwa serikali jumuishi, ambalo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ililipa kipaumbele tangu mwanzo wa utawala wa serikali ya muda ya Taliban, si njozi wala ndoto, bali ni juhudi za kutaka kutumia uwezo wote wa Afghanistan katika njia ya ustawi, amani na utulivu.