WFP: Watu milioni 2.5 wanakabiliwa na baa la njaa nchini Sudan

Takriban watu milioni 2 hadi milioni 2.5 wanatarajiwa kutumbukia kwenye janga la njaa nchini Sudan katika miezi michache ijayo kwa sababu ya vita vinavyoendelea nchini humo.

Onyo hilo lilitolewa Jumatano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa mjini Roma Italia na Port Sudan, hii itafanya hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula Sudan kufikia rekodi ya juu kabisa huku kukiwa na watu milioni 19 ambao ni theluthi mbili ya watu wote nchini humo wakiwa wameathirika.

Majimbo yanayotarajiwa kuathirika zaidi ni Darfur Magharibi, Kordofan Magharibi, Blue Nile, Red Sea na Darfur Kaskazini. Hivi karibuni pia Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa alitangaza habari hiyo ya kutisha Ijumaa na kuongeza kuwa watu milioni 19 nchini humo wanaweza kukumbwa na uhaba wa chakula katika miezi ijayo.

Wakati huohuo Kamishina mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema zaidi ya watu 150,000 sasa wamekimbia Sudan ambao ni raia wa Sudan pamoja na wakimbizi waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika nchi hiyo. Shirika la WFP linasema bei ya chakula imeongezeka maradufu katika nchi nzima na sasa bei ya kikapu kimoja cha chakula inatazamiwa kupanda kwa asilimia 25 katika miezi mitatu hadi sita ijayo.

Kutokana na mapigano yanayoendelea wakulima wengi inasema WFP hawawezi kwenda mashambani mwao kupanda mazao ya kilimo katika msimu wa mvua kati ya Mei na Julai hali ambayo itapandisha hata zaidi bei za vyakula.

Mapigano makali yalizuka Aprili 15 kati ya kiongozi mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye anaongoza jeshi la kawaida, na naibu wake aliyegeuka mpinzani Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Hadi sasa watu wasiopungua 700 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *