Balozi wa Yemen nchini Iran amepongeza uungaji mkono usioyumba wa Jamhuri ya Kiislamu kwa nchi hiyo masikini ya Kiarabu kwa muda wote wa uvamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na kusisitiza kuwa ni Iran pekee ndiyo ilisimama pamoja na watu wa Yemen katika nyakati ngumu.
Ibrahim Mohammad al-Deilami alisema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Iran la Mehr siku ya Jumapili. Katika mahojiano hayo amebainisha nafasi ya nchi mbalimbali katika vita vya muungano wa Saudia dhidi ya Yemen.
Deilami amesema “Nchi nyingi zinashiriki katika uvamizi wa Saudia na Marekani dhidi ya nchi yetu, isipokuwa nchi moja, ambayo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Ameongeza kuwa, “Iran ilisimama upande wa watu wa Yemen na kuwaunga mkono kwa dhati na kuwasilisha suala la Yemen kwa ikhlasi katika vikao vya kimataifa, na Wayemen hawakuona chochote isipokuwa msaada kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”
Akisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu tangu siku ya kwanza imetoa wito wa kukomesha uchokozi, kuondoa vikwazo, kupeleka misaada ya kibinadamu Yemen na kutoingilia masuala yake ya ndani, Balozi huyo amesema: “Iran ilisimama na watu wa Yemen kwa namna tofauti na katika ngazi zote. Hii ndiyo misimamo thabiti na ya uaminifu ya Iran tangu siku ya kwanza hadi sasa.”
Deilami amekanusha vikali madai kwamba harakati ya muqawama ya Ansarullah ya Yemen inapokea silaha na zana za kijeshi kutoka Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema “kufuatia uvamizi, si Ansarullah pekee, bali watu wote wa Yemen kutoka madhehebu, mikoa, makabila, vyama na nguvu zote za kisiasa wanashiriki. Vikosi vya wavamizi vinavyoongozwa na Saudi Arabia na wafuasi wake vimejaribu kudhoofisha muqawama na mapambano ya watu na kufanya ionekane kuwa kila kitu nchini Yemen kiko chini ya udhibiti wa Iran.”
Akisisitiza kwamba uhusiano kati ya Iran na Yemen hauegemei tu kwenye diplomasia bali pia uhusiano wa kihistoria na kidini, Deilami amesema: “Nchi zote mbili ziko katikati ya mapambano na muqawama dhidi ya mradi wa Wazayuni na Marekani.”
Deilami amesema, “Saudi Arabia inajaribu kusingizia kupitia vyombo vyake vya habari kwamba suala la kumaliza vita hilo liko mikononi mwa Wamarekani, na bila shaka hii ni kweli na Wamarekani wanashiriki katika uchokozi na ukatili huu, lakini ikiwa Riyadh itakuwa mwaminifu, inaweza kusitisha vita.” Saudi Arabia iliivamia Yemen mwaka 2015 ili kuiondoa Ansarullah madarakani lakini imeshindwa kufikia lengo hilo na sasa imetangaza azma yake ya kuhitimisha vita.