UN yatenga dola milioni 5 kuisaidia Misri kuwahudumia wakimbizi wa Sudan

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kukabiliana na Masuala ya Dharura (CERF) umesema kwamba umetenga dola milioni 5 za Kimarekani ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kibinadamu za kuisaidia Misri kuwahudumia watu wanaokimbia migogoro katika nchi jirani ya Sudan.

Katika taarifa yake, shirika hilo limesema, fedha hizo zitatumika kununulia chakula, maji na usafi wa mazingira, huduma za afya, kugawa fedha taslimu, kuwasaidia wakimbizi kisaikolojia na na masuala mengine ya kijamii. Fedha hizo ni maalumu kwa wale wakimbizi wanaotafuta hifadhi na raia wa nchi za kigeni walioko Sudan pamoja na jumuiya zinazopokea watu hao nchini Misri.

Tangu mzozo wa Sudan ulipozuka tarehe 15 mwezi uliopita wa Aprili, Misri imeshapokea idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Sudan.

Taarifa ya CERF pia imesema, zaidi ya watu 113,000 wamevuka mpaka wa Sudan na kuingia Misri kuanzia Mei 17, na idadi inaendelea kuongezeka huku takriban watu 5,000 wakiendelea kuingia nchini Misri kila siku wakitokea Sudan.

Kwa upande wake, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limekadiria kuwa, watu 350,000 wataingia Misri kutoka Sudan katika muda wa miezi sita ijayo.

Mbali na dola milioni 5 zilizotengwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuisaidia Misri kuhudumia wakimbizi wa Sudan, shirika la CERF pia limetenga dola milioni 17 kwa ajili ya kuzisaidia nchi nyingine jirani na Sudan, ikiwa ni pamoja na Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Sudan Kusini.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *