Matusi ya ubaguzi wa rangi yaliyotolewa dhidi ya mwanasoka wa Brazil Vinícius Júnior katika ligi ya soka ya Uhispania yamekosolewa na kulaaniwa vikali na viongozi wa nchi, makocha na nyota mbalimbali wa mchezo huo unaopendwa zaidi duniani kote.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, wakati wa mechi ya kandanda kati ya Real Madrid na Valencia iliyochezwa Jumapili usiku, Vinícius Júnior, mwanasoka wa Brazil anayechezea timu maarufu ya Real Madrid, alilengwa na matusi ya kibaguzi ya mashabiki wa Valencia kwenye uwanja wa Mestalla nchini Uhispania.
Kulingana na mikanda ya video iliyorekodiwa ndani ya uwanja, kauli za matusi ya ubaguzi ya rangi ya kumwita mwanasoka huyo “kima” zilikaririwa mara kadhaa wakati wa mechi, mpaka wakati mmoja Vinícius akaamua kuelekea kwenye jukwaa la watazamaji kupambana na shabiki mmoja.
Mechi hiyo haikusimamishwa na mwamuzi na hatimaye mchezaji huyo Mbrazil alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kitendo kisicho cha kimichezo katika dakika ya 90+7 baada ya tukio la ugomvi baina yake na mchezaji mwenzake kukaguliwa kwa kutumia video ya kumsaidia mwamuzi, VAR.
Baada ya mechi hiyo, Vinícius mwenye umri wa miaka 22 na anayetambulika kama mmoja wa wanasoka nyota duniani hivi sasa aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, Uhispania, sasa inajulikana “kama nchi ya wabaguzi wa rangi” huko Brazil na akaongeza kuwa “ubaguzi wa rangi ni jambo la kawaida katika La Liga”.
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, ametoa wito kwa FIFA na La Liga kuchukua “hatua kali” baada ya matukio ya Jumapili kwenye uwanja wa Mestalla wa Valencia na akasema “hatuwezi kuruhusu ufashisti na ubaguzi wa rangi uchukue udhibiti wa viwanja vya soka”.
Klabu ya soka ya Real Madrid imetoa taarifa ya kulaani vikali matusi ya ubaguzi wa rangi yaliyoelekezwa kwa mchezaji wake na kuyaelezea matusi hayo kuwa ni “uhalifu wa chuki”.
Ligi ya Uhispania imeshawasilisha malalamiko tisa rasmi yanayohusiana na matusi ya ubaguzi wa rangi sawa na ya siku ya Jumapili yaliyotolewa dhidi ya Vinícius katika misimu miwili iliyopita, lakini mengi yao hayajashughulikiwa.
Akizungumza baada ya mechi ya Jumapili, meneja Mtaliano wa Real Madrid Carlo Ancelotti, ameielezea hali hiyo kwa kusema: “hakuna kitakachofanyika, kwa sababu hili tayari limefanyika mara kadhaa katika viwanja vingine na hakuna kilichofanyika”.
Vinícius ameungwa mkono pia na wachezaji wenzake akiwemo kipa Thibaut Courtois ambaye amesema alisikia “kelele za kima” baada ya takriban dakika 20 za mchezo, na akasisitiza kwamba, angeungana na mchezaji mwenzake huyo kutoka uwanjani kama angeamua kutoendelea na mchezo.
Mshambuliaji nyota wa Ufaransa Kylian Mbappé yeye ameandika ujumbe wa kumfariji Vinicius kwa kumwambia: “Huko peke yako.”
Rais wa FIFA, Gianni Infantino naye pia ameonyesha mshikamano kamili na Vinícius, ambaye amekuwa akicheza kandanda nchini Uhispania kwa miaka mitano sasa akisema. “hakuna nafasi ya ubaguzi wa rangi katika soka au katika jamii; na Fifa inasimamia wachezaji wote ambao wamejikuta katika hali kama hii”.
Ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji huyo Mbrazil umewakasirisha pia wachezaji kadhaa wa zamani wa soka. Beki wa zamani wa Uingereza Rio Ferdinand amehoji, “ni mara ngapi zaidi Vinícius akabiliwe na mambo kama haya. Ninaona uchungu, ninaona karaha, ninahisi anahitaji msaada … na viongozi hawafanyi lolote”.
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil Ronaldo, ambaye alitumia misimu mitano kuichezea Real Madrid miaka ya 2000, amesema: “Kesi nyingine ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinícius katika ligi ya Uhispania. Mpaka lini? Maadamu kuna hali ya kutokujali, kutakuwapo na ubaguzi wa rangi.”
Nchini Brazil kwenyewe, taa za sanamu maarufu la Kristo Mkombozi la nchini humo nazo pia zilizimwa hapo jana kuonyesha mshikamano na Vinicius Jr.
Taa za nembo hiyo ya kitaifa ya Brazil iliyoko Rio de Janeiro, jimbo alikozaliwa Vinicius mwenyewe, zilizimwa kwa muda wa saa nzima mnamo saa kumi na mbili jioni kwa saa za huko ambapo serikali ya Brazil na ulimwengu wa kandanda waliungana kulaani vitendo vya ubaguzi wa rangi vilivyotokea kwenye mechi ya ligi ya Uhispania siku ya Jumapili usiku…/