Sheria dhidi ya LGBTQ Uganda yamkasirisha rais wa Marekani, atishia kuiwekea nchi hiyo vikwazo

Rais Joe Biden wa Marekani amelaani sheria mpya iliyotiwa saini na Rais Yoweri Museveni wa Uganda dhidi ya vitendo vya ushoga na kusema kuwa Marekani inaweza kuiwekea Uganda vikwazo huku akitoa wito wa sheria hiyo kufutwa mara moja.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, watu wanaoshiriki kwenye vitendo vya liwati na usagaji watatumikia hadi kifungo cha maisha jela.

Biden amesema, ameliagiza Baraza la Usalama wa Taifa la Ikulu ya Marekani litathmini athari za sheria hiyo katika nyanja zote za ushirikiano wa nchi hiyo na Uganda, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa Marekani kusitisha kutoa huduma za usalama chini ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kusaidia maambukizi ya UKIMWI, (PEPFAR) na aina nyingine za msaada na uwekezaji.

Vilevile Rais wa Marekani ameeleza kwamba, serikali yake itazingatia athari za sheria hiyo kama sehemu ya mapitio yake ya kustahiki kwa Uganda kwa Sheria za Ukuaji na Fursa ya Afrika (AGOA).

Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, mara nyingi hutumia silaha ya vikwazo dhidi ya nchi na mataifa yenye misimamo huru na yanayohalifu kufuata sera za nchi hizo.

Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among alitangaza na kuthibitisha jana Jumatatu kwamba, Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni amepasisha rasmi sheria ya kupiga marufuku nchini humo na kuwachukulia hatua kali wanaojihusisha na mahusiano ya kingono ya watu wa jinsia moja kwa mujibu wa Sura ya 91(3)(a) ya Katiba ya Uganda ya Mwaka 2015.

Among alisema: “Tumesimama kidete kulinda utamaduni, thamani na maazimio ya taifa letu, kwa mujibu wa malengo yetu ya taifa nambari 19 na 24, na pia kwa mujibu wa kanuni za sera zetu. Wananchi wa Uganda wamezungumza, na ni jukumu letu kuitelekeza sheria hii kwa uadilifu, kwa dhati na kwa njia madhubuti.”

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amekuwa mstari wa mbele kulaani vikali mahusiano ya jinsia moja kwa muda mrefu, na mwaka 2013 alitia saini sheria ya kukabiliana na ufuska huo licha ya mashinikizo na vitisho vya nchi za Magharibi.

Wakati huohuo, vyombo vya habari nchini Uganda vimetangaza kuwa serikali ya Marekani imefuta viza ya kuingia nchini humo ya Spika wa Bunge  la Uganda Anita Among…/

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *