Rais Vladimir Putin wa Russia amesema mgogoro katika soko la chakula duniani hauna uhusioano wowote na operesheni za kijeshi za nchi hiyo huko Ukraine, kwa sababu mgogoro huo ulibuniwa muda mrefu kabla ya vita vya Ukraine.
Baada ya kuanza vita kati ya Russia na Ukraine, usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine kama chanzo kikuu cha bidhaa hiyo ulimwenguni ulikabiliwa na matatizo na uuzaji wa bidhaa za kilimo za Russia pia umesimamishwa kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi.
Nchi hizo zinaituhumu Russia kuwa ndiyo imesababisha mzozo wa chakula duniani kwa kuishambulia Ukraine.
Katika kikao na viongozi na wawakilishi wa nchi za Kiafrika, Rais Vladimir Putin alisema jana Jumamosi kuwa mgogoro wa chakula duniani unatokana na hatua zisizo za kiadilifu za kiuchumi zinazotekelezwa na nchi za Magharibi ikiwemo Marekani kwa ajili ya kutatua matatizo yao na hasa katika kipindi cha kuenea janga la virusi vya corona.
Wakati huo huo Rais Putin alitangaza Jumanne iliyopita kwamba Russia inafikiria kujiondoa katika makubaliano ya mauzo ya nafaka ya Bahari Nyeusi.
Ameongeza kuwa sehemu kubwa ya nafaka ya Ukraine, inapelekwa katika nchi tajiri za Ulaya, kinyume na makubaliano hayo.
Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia alisema Alhamisi kwamba kurefushwa makubaliano ya nafaka hakuwezi kujadiliwa kabla ya kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa huko nyuma.
Sergei Vershinin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia amesema licha ya kupita karibu mwaka mmoja baada ya kusainiwa makubaliano ya usafirishaji wa nafaka ya Bahari Nyeusi huko Istanbul, usafirishaji wa mbolea ya amonia ya Russia haujafanyika.
Ameongeza kuwa bila kutatuliwa tatizo hilo, hatuwezi kuzungumzia kurefushwa mpango wa Bahari Nyeusi baada ya Julai 17.
Soko la kimataifa la nafaka linakabiliwa na matatizo mengi kufuatia vita vya Ukraine. Russia na Ukraine ni miongoni mwa nchi zinazozalisha na kuuza kwa wingi nafaka duniani.
Mnamo Julai 22, 2022, Uturuki, Ukraine, Russia na Umoja wa Mataifa zilitiliana saini huko Istanbul hati ya kuwezesha kusafirishwa salama nafaka na chakula kutoka bandari za Ukraine.
Makubaliano hayo yalirefushwa kwa muda wa miezi miwili Mei 17 mwaka huu.